Usyk, Dubois kumaliza ubishi Wembley
Muktasari:
- Hili siyo pambano la kawaida, bali ni fursa ya kihistoria kwa mmoja wao kuandika upya jina lake katika orodha ya mabondia wakubwa zaidi wa wakati wote.
SIKU zinawadia. Uwanja wa Wembley, jijini London, unatarajiwa kuwa kitovu cha dunia ya ngumi Julai 19, 2025, wakati mabondia wakubwa Oleksandr Usyk na Daniel Dubois watakapoingia ulingoni kwa pambano la marudiano la ubingwa wa dunia wa uzito wa juu.
Hili siyo pambano la kawaida, bali ni fursa ya kihistoria kwa mmoja wao kuandika upya jina lake katika orodha ya mabondia wakubwa zaidi wa wakati wote.
Oleksandr Usyk, ambaye ni raia wa Ukraine, ana rekodi ya kushinda mapambano yote 23 aliyopigana na 14 kati ya hayo alishinda kwa KO.
Amekuwa bingwa wa dunia katika uzito wa kati (cruiserweight) na baadaye katika uzito wa juu, na anarejea Wembley akiwa bingwa wa mikanda ya WBA, WBO na WBC baada ya kumshinda Tyson Fury katika pambano la kusisimua Mei 2024.
Kwa upande mwingine, Dubois, ambaye ni raia wa Uingereza mwenye rekodi ya kushinda mapambano 22 na kupoteza mawili, amekuwa akipanda chati kwa kasi.
Mwaka 2023 alipoteza mbele ya Usyk kwa TKO katika raundi ya tisa. Baada ya hapo, Dubois alirudi kwa kishindo kwa kumshinda Anthony Joshua na kunyakua taji la IBF lililokuwa na sasa ana nafasi ya kulipa kisasi mbele kwa Usyk.
Mbali ya pambano hili ambalo litahudhuriwa na mashabiki takribani 90,000, pia kutakuwa na mapambano ya utangulizi mawili ambayo ni ubingwa wa dunia wa uzito wa cruiser lile la Lawrence Okolie dhidi ya Kevin Lerena.
Pia kutakuwa na pambano la uzito wa juu la England kati ya Viktor Vykhryst na Frazer Clarke.
Matangazo ya pambano hili yanatarajiwa kuanza saa 6:45 usiku kwa saa Afrika ya Mashariki.
Wataalamu wengi wa mchezo huu wanampa nafasi Usyk kutokana na uzoefu na historia yake ya kutopigwa, lakini wengine wanaamini Dubois anaweza kuleta mshangao, hasa kwa nguvu na hasira aliyonayo juu ya kutaka kulipa kisasi.
Derek Chisora, ambaye ni bondia mkongwe wa Uingereza, alisema: “Dubois anahitaji kuwa pepo kichaa (crazy demon) ili kumshinda Usyk.”