Kiungo Mamelodi Sundowns, Jayden Adams afariki dunia
Muktasari:
- Kiungo huyo hivi karibuni aliiwakilisha Afrika Kusini katika Kombe la Dunia la FIFA, ambako timu yake ilitolewa mapema.
Vyombo vya habari Afrika Kusini vimeripoti taarifa za kifo cha kiungo wa Bafana Bafana na Mamelodi Sundowns, Jayden Adams, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 25.
Kiungo huyo hivi karibuni aliiwakilisha Afrika Kusini katika Kombe la Dunia la FIFA, ambako timu yake ilitolewa mapema.
Hadi sasa, taarifa kuhusu chanzo cha kifo chake bado hazijawekwa wazi.
Chombo cha Habari cha Siya Crew kimesema kuwa kimezungumza na wawakilishi wa mchezaji huyo pamoja na mlezi wake, ambao wamethibitisha taarifa hizo za kusikitisha.
Mamelodi Sundowns pia ilitafutwa kuzungumzia suala hilo, lakini haijathibitisha wala kukanusha taarifa hizo, ikisisitiza kuwa familia iachiwe nafasi ya faragha katika kipindi hiki kigumu.
Brendine Johnson, ambaye alikuwa mlezi na mshauri wa Adams, alizungumza kwa niaba ya familia na kueleza kwa kile kilichotokea.
"Kwa sasa maumivu bado ni makubwa. Familia haiko tayari kupokea simu wala kuzungumza na mtu yeyote. Kifo hiki kimetuumiza sana. Alikuwa amerudi tu kutoka Kombe la Dunia, halafu tukapata habari hizi za kusikitisha. Nilizungumza naye Alhamisi iliyopita, alikuwa na matumaini makubwa ya kurejea kambini baada ya Kombe la Dunia. Akiwa bingwa wa CAF, alikuwa anafahamu changamoto zilizokuwa mbele yake na alikuwa amejiandaa kikamilifu. Alikuwa mtu anayependa kutumia muda wake akiwa nyumbani pamoja na familia yake.
"Kwa sasa sina maneno ya kuelezea maumivu haya. Tunawaomba watu waheshimu faragha ya familia. Ninathibitisha kwamba kweli amefariki dunia. Hakuna aliyetarajia jambo hili," alisema Johnson.
Adams alijijengea jina akiwa Stellenbosch FC kabla ya kuhamia Mamelodi Sundowns na kupata nafasi katika timu ya taifa ya Afrika Kusini, Bafana Bafana. Kiwango chake bora katika Kombe la Dunia kilidhihirisha ukuaji wake na umuhimu wake katika soka la kiwango cha juu.
Taarifa zaidi kuhusu msiba huo zitatolewa kadiri zitakavyopatikana, huku faragha ya familia ikiendelea kuheshimiwa katika kipindi hiki cha maombolezo.