Ndani ya penzi la Kvaratskhelia na Nitsa lililomjengea bingwa wa UEFA
Muktasari:
- Kvaratskhelia ambaye amekuwa pamoja na Nitsa tangu mwaka 2021, alikuwa sehemu ya kikosi cha PSG kilichoifunga Arsenal kwa mikwaju ya penalti 4-3 katika fainali ya UEFA iliyochezwa katika dimba la Puskas Arena, Hungary.
Miongoni mwa waliompongeza Khvicha Kvaratskhelia, 25, baada ya kutwaa taji la UEFA msimu uliopita akiwa na Paris Saint-Germain (PSG), ni pamoja na mkewe Nitsa Tavadze, 24, ambaye alimtaja mchezaji huyo kama bingwa wake wa muda wote.
Kvaratskhelia ambaye amekuwa pamoja na Nitsa tangu mwaka 2021, alikuwa sehemu ya kikosi cha PSG kilichoifunga Arsenal kwa mikwaju ya penalti 4-3 katika fainali ya UEFA iliyochezwa katika dimba la Puskas Arena, Hungary.
"Natamani watu waelewe ni nguvu kiasi gani zinahitajika kufikia mafanikio kama haya, licha ya presha na matarajio makubwa bado uliendelea kupambana kila siku na sasa wewe ni bingwa wa UEFA mara mbili mfululizo.
"Limekuwa jambo la kupendeza zaidi kushuhudia ukitimiza kila ndoto ambayo uliwahi kuiombea. Siku zote ninajivunia sana wewe, ninakupenda bingwa wangu wa milele. Bado mengi mazuri yanakuja," alieleza Nitsa.
Kvaratskhelia ni mmoja wa wachezaji wenye vipaji vikubwa zaidi vya soka duniani kwa sasa, winga huyo kutoka Georgia amewavutia mashabiki wengi kwa uwezo wake wa kupiga chenga, kasi kubwa na uwezo wa kufunga mabao.
Kadiri anavyoendelea kung'ara uwanjani, ndivyo na mashabiki wengi wamekuwa na hamu ya kutaka kujua kuhusu maisha yake binafsi, hasa upande wa ndoa yake na Nitsa Tavadze. Je, ni lini na wapi wawili hao walikutana hadi kuja kuoana?.
Kwa mara ya kwanza Kvaratskhelia na Nitsa walikutana mwaka 2021 baada ya kukutanishwa na rafiki yao wa karibu, licha ya kufahamiana siku hiyo lakini uhusiano rasmi ulikuja kuanza takribani mwezi mmoja baadaye, na mengine sasa ni historia.
Mara ya kwanza kuonekana hadharani wakiwa pamoja ilikuwa katika mechi ya mpira wa kikapu kati ya Italia na Georgia. Agosti 2022, ndipo Kvaratskhelia alithibitisha katika mahojiano alikuwa kwenye uhusiano na Nitsa.
Wakati huo, Kvaratskhelia alikuwa akiichezea Napoli ya Italia, huku Nitsa akiendelea na masomo yake ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Tbilisi.
Kutokana na masomo yake, Nitsa hakuweza kuhamia Italia kwa wakati huo ili kuishi na pamoja na Kvaratskhelia lakini kipindi cha likizo alikuwa akisafiri kwenda Napoli kumshangilia mchezaji huyo kwenye mechi za klabu hiyo, jambo ambalo kilimpa furaha sana hadi wakati mwingine kulia uwanjani.
Simulizi ya uhusiano wao inaonyesha hata katika maisha yenye ratiba nyingi na shughuli za kuchosha, bado upendo wa kweli unaweza kudumu na kustawi.
Hatimaye Oktoba 16, 2023, Kvaratskhelia na Nitsa walifunga ndoa katika nyumba ya watawa ya Samtavro iliyopo Mtskheta nchini Georgia.
Katika sherehe hiyo walifuata mila za kwao kwa kuvaa mavazi ya kitamaduni. Pia walipita chini ya upanga ulioshikiliwa na watu 12, ikiwa ni ishara ya heshima na ulinzi katika utamaduni wao.
Harusi hiyo ilihudhuriwa na ndugu wa karibu pamoja na marafiki wachache, na baadaye Kvaratskhelia aliposti picha za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii akiambatanisha na maelezo mafupi: "16.10.23" pamoja na emoji ya upendo.
Hata hivyo, licha ya ndoa yao, Nitsa aliendelea kuishi Georgia ili kuendelea na masomo yake ya udaktari. Kipindi hicho Kvaratskhelia alikuwa akipokea mshahara wa takribani Pauni 1.3 milioni (Sh4.5 bilioni) kwa mwaka kutoka Napoli.
Mapenzi yao yalizidi kuimarika na kujawa na furaha pindi walipopata mtoto wao wa kwanza ambaye alizaliwa Agosti 21, 2024, mtoto huyo wa kiume alipewa jina la Damiane.
Kvaratskhelia aliwafahamisha mashabiki kuhusu kuzaliwa kwa mtoto huyo katika kurasa zake za mitandao ya kijamii akieleza jinsi alivyofurahia kuwa baba kwa mara ya kwanza katika maisha yake.
Hata hivyo, ingawa Kvaratskhelia huwa hapendi kuweka wazi maisha yake binafsi mtandaoni, mara chache amekuwa akiposti picha za familia yake akionyesha upendo kwa mkewe na mtoto wake.
Vilevile, Nitsa hufanya hivyo katika ukurasa wake wa Instagram ambao una wafuasi zaidi ya 211,000, asilimia kubwa ya mashabiki hao ni wa mumewe pamoja na klabu anayoichezea kwa sasa, yaani PSG.
Hivyo hadi sasa ni wazi safari yao kutoka uchumba hadi ndoa na sasa wakiwa wazazi, inaonyesha jinsi walivyoweza kusimama pamoja katika kila hatua muhimu waliyopiga katika maisha yao. Safari yao imekuwa mfano wa upendo wa kweli na wenye kujitolea kwa lengo la kufanisha kitu kizuri maishani.