Usipokunywa bia haufi

DOHA, QATAR. RAIS wa FIFA, Gian Infantino amesema kutokuwepo kwa bia kwenye viwanja vya michuano ya Kombe la Dunia inayotarajiwa kuanza kesho huko Qatar ni safi tu.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari unaoendelea huko nchini Qatar, Infantino amesema mtu asipokunywa bia kwa masaa mawili au matatu haiwezi kuwa shida sana.

"Usipokunywa bia kwa masaa mawili matatu, unaweza kuishi, kwa sababu utaratibu huu pia upo hata kwenye nchi za Ulaya, ukienda Ufaransa, Ureno hata Uswiss, hakuna masuala ya  kuuza bia viwanjani."

Katika taarifa iliyotolewa na mamlaka nchini Qatar ilieleza wazi kwamba hakutakuwa na pombe yoyote itakayouzwa ndani ya viwanja nane vitakavyotumika kwenye michezo mbali mbali.

Infantino amesema anajisikia vibaya kwa washirika wao wa kampuni za pombe lakini hiyo ni changamoto tu kwenye kazi yoyote.

"Tumepambana ili pombe ziwepo lakini tumeshindwa, sijui kwanini, inawezekana ni kutokana na kwa sababu ni nchi ya kiislamu."

Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kesho saa 1:00 usiku, ambapo mwenyeji Qatar atacheza mechi ya ufunguzi dhidi ya Ecuador.