Usipojipanga, unapangwa.. moto wa Qatar; Neymae, Ronaldo, Suarez na Partey

DOHA, QATAR. NA leo tena. Ni mchakamchaka wa fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar, ambapo Granit Xhaka, Eric-Maxime Choupo Moting, Thomas Partey, Luis Suarez, Neymar na Son Heung-min watawashiana moto kuonyeshana nani ni nani kwenye kinyang’anyiro hicho cha kusaka ubingwa wa dunia.

Leo, Alhamisi ni zamu ya Kundi G na Kundi H kucheza mechi za kwanza, ambapo patashuhudia vigogo wawili wanaopewa nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa wa fainali hizo, Brazil ya mkali Neymar na Ureno ya supastaa Cristiano Ronaldo.

Afrika pia itarusha kete yake nyingine, wakati Cameroon watakapokuwa mzigoni kuwakabili Uswisi katika mchezo wa mapema kabisa kwenye Kundi G, kabla ya Brazil kumaliza ubishi dhidi ya Serbia ya staa Dusan Tadic.

Macho ya wengi yatakuwa kwenye kipute cha Brazil kuona kama kuna kitu watafanya kwenye fainali hizo, watakaporusha kete yao ya kwanza huko Qatar. Brazil, ambao ni mabingwa wa kihistoria wakinyakua taji la dunia mara tano, kikosi chao kimesheheni mastaa wengi wanaofanya vyema kwenye soka la dunia kwa sasa, akiwamo supastaa Neymar.

Neymar anafahamu kilichomkuta swahiba wake Lionel Messi wanaocheza pamoja Paris Saint-Germain baada ya chama lake la Argentina kukumbana na kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Saudi Arabia juzi Jumanne. Brazil na Serbia zimeshawahi kukutana mara mbili, Kombe la Dunia 2018, ambapo Brazil ilishinda 2-0, huku mechi nyingine ilikuwa ya kirafiki, 2014 - Brazil ilishinda pia bao 1-0. Patachimbika.

Katika mchezo mwingine wa Kundi hilo, Cameroon yenye mkali Choupo Moting itakuwa na shughuli kukipiga na Uswisi ya Xhaka. Mashabiki wa soka wa Afrika wanasubiri kuona wawakilishi wa bara hilo kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia wakipata ushindi. Uswisi inafahamu vyema makali ya timu za Kiafrika baada ya kuchapwa na Ghana mabao 2-0 katika mechi ya kirafiki.

Mziki utakuwa kwenye Kundi H, ambapo Uruguay itakapokuwa na kazi nzito mbele ya Korea Kusini kabla ya Ureno kuwakabili Ghana.

Uruguay na Korea Kusini ni vita ya Suarez na Son. Uruguay na Korea Kusini zimeshawahi kukutana mara kadhaa, lakini mbili za mwisho, kila moja ilishinda mara moja. Nani atatoboa? Kuhusu Kombe la Dunia, zilikutana 2010 huko Afrika Kusini, ambapo Uruguay iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Supastaa Ronaldo baada ya kumshuhudia mpinzani wake wa miaka mingi, Messi akipoteza mchezo wa kwanza - yeye atakuwa kwenye shughuli pevu kuwakabili wakali wa Afrika, Black Stars. Je, Ronaldo - ambaye atacheza mechi hiyo akiwa mchezaji huru ataweza kutoboa mbele ya kikosi chenye mkali matata kabisa, kiungo wa mpira, Partey?

Ureno na Ghana zilishawahi kupangwa kundi moja kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Brazil 2014, ambapo mchezo huo wa Kundi G ulimalizika kwa chama la Ronaldo kushinda 2-1.

Ureno ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kubeba ubingwa kwenye fainali hizo za Qatar baada ya kikosi chao kusheheni mastaa wa maana akiwamo Bruno Fernandes, Bernardo Silva, Joao Cancelo na Joao Felix. Fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar, usipojipanga utapangwa.