Usiku wa maamuzi UCL, Arsenal, Man City, Chelsea vitani
Muktasari:
- Mvuto wa michezo hiyo unatokana na matokeo ya mechi za mkondo wa kwanza na baadhi ya timu zinaingia zikiwa na faida ya ushindi huku nyingine zikihitaji kufanya kazi ya ziada ili kupindua matokeo na kusonga mbele.
LONDON, ENGLAND: Macho na masikio ya mashabiki wa soka yako leo Jumanne usiku na zitapigwa mechi nne za hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, zikitarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kati ya miamba nane itakayokutana.
Mvuto wa michezo hiyo unatokana na matokeo ya mechi za mkondo wa kwanza na baadhi ya timu zinaingia zikiwa na faida ya ushindi huku nyingine zikihitaji kufanya kazi ya ziada ili kupindua matokeo na kusonga mbele.
Katika mechi za leo, klabu tatu za England, Arsenal, Manchester City na Chelsea zitacheza nyumbani, lakini mbili kati yao zina kibarua kigumu cha kubadili matokeo ya mechi za kwanza. Ni usiku ambao unaweza kuamua hatma ya baadhi ya timu na kuandika historia mpya katika soka la Ulaya.
Katika Uwanja wa Emirates, Arsenal itaikaribisha Bayer Leverkusen ikiwa katika kiwango kizuri baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Everton mwishoni mwa wiki katika Ligi Kuu England. Ushindi huo umeongeza rekodi yao ya kutopoteza mechi 13 za mashindano yote.
Chini ya Kocha Mikel Arteta, Arsenal imekuwa imara nyumbani katika michuano ya Ulaya, ikipoteza mechi moja tu kati ya 16 zilizopita za mashindano hayo.
Kwa upande wa Leverkusen, inaingia ikiwa haijapoteza katika mechi sita zilizopita za mashindano yote. Kocha Kasper Hjulmand ana matumaini ya kuendeleza uimara wa safu ya ulinzi ambayo haijaruhusu bao katika mechi nne zilizopita ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mechi ya kwanza zilipokutana ilimalizika kwa sare ya 1-1, huku Kai Havertz akiifungia Arsenal na Robert Andrich akifunga kwa upande wa Leverkusen.
Kwa upande mwingine, Chelsea inahitaji ushindi wa angalau mabao 3-0 dhidi ya Paris Saint-Germain baada ya kupoteza mechi ya kwanza kwa mabao 5-2.
Hata hivyo, matokeo ya hivi karibuni hayatoi matumaini makubwa baada ya kushinda mechi moja tu kati ya sita zilizopita, huku kipigo cha 1-0 kutoka Newcastle United mwishoni mwa wiki kikiongeza presha kwa kikosi hicho.
Katika Uwanja wa Etihad, Manchester City itakuwa na kibarua kigumu cha kupindua matokeo baada ya kupoteza 3-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya Real Madrid. Matokeo hayo yanaifanya City kuhitaji ushindi wa mabao matatu ili kusonga mbele. Sare ya 1-1 dhidi ya West Ham United mwishoni mwa wiki inaonyesha bado wanatafuta kurejea kwenye makali yao.
Kocha Pep Guardiola alikiri kazi waliyonayo si rahisi dhidi ya Real Madrid, ambao wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na morali kubwa baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Elche CF katika ligi ya Hispania.
Nchini Ureno, Sporting CP inachangamoto ya kupindua matokeo baada ya kufungwa mabao 3-0 na FK Bodø/Glimt katika mchezo wa kwanza. Sporting inategemea nguvu yao nyumbani walikoshinda mechi 15 mfululizo, lakini Bodø/Glimt tayari wameandika historia kwa kufika hatua hii ikiwa inashiriki kwa mara ya kwanza katika michuano hii na ikikaribia kufuzu robo fainali.