UNAZINGUA : Vieira amlalamikia Wenger,atoa onyo

Muktasari:

  • Patrick Vieira, mmoja kati ya wachezaji wa shoka kucheza chini ya Wenger akiwa amenunuliwa na kocha huyo kwa dau la Pauni 3 milioni akitokea AC Milan mwaka 1996 amedai kwamba, kikosi cha sasa cha Wenger kina wachezaji wengi walaini na itakuwa ngumu kwao kuchukua ubingwa wa England.

Stoke,England. WAKATI huo Arsenal ikiwa na wachezaji wababe ilikuwa inavutia kuitazama. Ilikuwa inashinda mechi nyingi kisha inashinda taji. Mmoja kati ya wachezaji wababe wa nyakati hizo amemvaa Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger kwa kudai kuwa wachezaji wa aina yake hawapo na ndiyo maana Arsenal isahau ubingwa.

Patrick Vieira, mmoja kati ya wachezaji wa shoka kucheza chini ya Wenger akiwa amenunuliwa na kocha huyo kwa dau la Pauni 3 milioni akitokea AC Milan mwaka 1996 amedai kwamba, kikosi cha sasa cha Wenger kina wachezaji wengi walaini na itakuwa ngumu kwao kuchukua ubingwa wa England.

Vieira, Mfaransa aliyezaliwa Senegal ambaye alikuwa nahodha wa Arsenal kikosi kilichotwaa ubingwa wa mwisho wa England msimu wa 2003-04 wakicheza mechi bila ya kufungwa akiwa amekaa klabuni hapo kuanzia mwaka 1996 mpaka 2005 amedai wachezaji wa kariba ya kikosi cha mwisho kutwaa ubingwa hawapo tena.

“Kizazi changu kilikuwa na wachezaji wengi wenye nguvu. Katika miaka mitano au sita iliyopita Arsenal imejaza wachezaji wengi wenye mbinu. Sisi ambao tulicheza msimu mzima bila ya kufungwa tulikuwa na kila kitu,” alisema Vieira ambaye pia alitwaa mataji mawili ya FA katika misimu yake mitatu ya mwisho Arsenal.

“Sasa hivi ninapoitazama Arsenal ikicheza, wanacheza mpira mzuri, lakini kuna kitu huwa wanakosa, hawana nguvu wala ari kubwa. Timu haifanyi vizuri kama ilivyokuwa zamani kwa sababu unahitaji kushinda mechi za soka. Wamekuwa wakiudhi na kufungwa mechi ambazo walipaswa kushinda,” aliongeza Vieira.

Vieira, ambaye kwa sasa ni kocha wa klabu ya New York City inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani, amemshangaa Wenger kwa kutowashirikisha wachezaji wengi wa zamani katika mabenchi yake ya ufundi huku akiamini vijana wadogo wangejifunza mengi kutoka kwa wachezaji wakongwe waliopita klabuni hapo.

“Nimeudhika sana wachezaji wa zamani wa Arsenal kutofanya kazi Arsenal. Ni jambo zuri kwa wachezaji wadogo kuwaona kina Thierry Henry, (Freddie) Ljungberg, au (Martin) Keown ambao wamefanya kazi klabuni kwa muda mfupi au wamefanya kazi kwingineko.”

“Nadhani wangeweza kufanya zaidi, wachezaji wanataka kufanya kazi lakini hawapewi nafasi. Sielewi kwa nini. Mfano halisi ni klabu ya Ajax. Unawaona wachezaji wote wa zamani wanafanya kazi klabuni, uwanjani au ofisini. Milango ipo wazi kwao. Lakini kwa Arsenal hawafanyi hivyo, sijui kwa nini.” Alihoji Vieira.

Amwonya Paul Pogba

Vieira alimgeukia kiungo wa kimataifa wa Ufaransa, Paul Pogba ambaye amenunuliwa kwa dau la pauni 89 milioni likiwa ni uhamisho wa dunia na kudai kwamba, staa huyo asijiweke katika anga za Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

“Mimi ni shabiki mkubwa wa Pogba. Nadhani ni mchezaji mzuri sana na hakuna shaka katika hilo. Lakini wakati huo huo naamini yupo katika Ligi tofauti na atakuwa katika presha kubwa sana kutokana na bei aliyonunuliwa na matazamio ya mashabiki,” alisema Vieira.

“Itabidi ashirikiane vyema na wenzake kwa sababu kama anaamini atashinda mechi mwenyewe basi litakuwa kosa kubwa kwake. Kama atajaribu kufanya kitu ambacho hawezi kufanya litakuwa kosa pia kwake.”

“Nilisoma kitu fulani kutoka kwa Mourinho kwamba atashinda mechi nyingi kama Messi au Ronaldo. Kama watu wanatazamia atafunga mabao 40 kwa msimu, jambo hilo haliwezi kutokea, lakini anaweza kuleta tofauti kwa nguvu zake na uwezo wake wa kiakilia,” aliongeza Vieira.