Thiago Silva aaga Chelsea kwa machozi

LONDON, ENGLAND. BEKI wa kati wa Chelsea, Thiago Silva, 39, amethibitisha huku akitokwa na machozi kwamba ataachana na miamba hiyo ya Stamford Bridge mwishoni mwa msimu.

Katika taarifa aliyoitoa kwa video kupitia tovuti ya klabu hiyo, Silva alisema: "Chelsea imebeba maana kubwa kwangu. Nilikuja hapa kwa lengo la kukaa mwaka mmoja tu lakini nimejikuta nikikaa miaka minne. Hii sio kwa ajili yangu tu ila kwa familia yangu pia.

"Watoto wangu wanachezea Chelsea ya vijana hivyo ni chanzo cha kujivunia kuwa sehemu ya familia ya Chelsea – pengine kwa sababu wanangu wa kiume wako hapa. Natumai wataendeleza maisha yao ya soka katika klabu hii ya washindi ambayo wachezaji wengi wanatamani kuwa sehemu ya kikosi. Nadhani katika kila nilichofanya kwa miaka minne hapa, nilijitoa kwa kila kitu.

"Lakini, kwa bahati mbaya, kila chenye mwanzo kina katikati na mwisho. Hilo halimaanishi kwamba huu ndio mwisho wangu hapa. Natumai ninaacha milango wazi ili miaka michache ijayo niweze kurejea, kwa nafasi nyingine tofauti ya ajira. Lakini... haya ni mapenzi yasiyoelezeka. Ninachoweza kusema tu ni asante.”

Chelsea ilimnasa beki huyo wa Kibrazili bure kabisa kutoka Paris Saint-Germain. Wakati huo Silva akiwa na umri wa miaka 36, alionekana kama angekuwa na wakati mgumu kwenye maisha ya Ligi Kuu England baada ya timu yake kuwa nyuma kwa mabao 3-0 dhidi ya West Brom kwenye mechi yake ya kwanza.

Lakini, Chelsea ilipambana na kupata sare ya mabao 3-3 na baada ya hapo, Chelsea iliruhusu nyavu zake kuguswa mara mbili tu katika mechi sita zilizofuatia ambazo Silva alianzishwa na msimu huo walikwenda kunyakua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuichapa Manchester City kwenye mchezo wa fainali.

Licha ya Mbrazili huyo kucheza mechi 151 kwenye michuano yote tangu wakati huo, alishinda pia Uefa Super Cup na Klabu Bingwa ya Dunia, lakini sasa amepoteza nafasi kwenye kikosi cha kwanza misimu ya hivi karibuni.

Na zaidi, mmiliki mpya wa Chelsea, Todd Boehly ameweka nguvu zaidi kwa wachezaji vijana, hivyo Silva hakuna namna zaidi ya kukubali tu matokeo kwa kukusanya virago vyake na kuondoka.

Chelsea itakipiga na Tottenham Hotspur, West Ham United, Nottingham Forest, Brighton na Bournemouth katika mechi zao tano zilizobaki kwenye Ligi Kuu England msimu huu utakaokwisha Mei 19.

Na kinachosemwa, Silva kwa sasa atarejea kwenye klabu yake ya zamani, Fluminense ya huko Brazil.