Unaambiwa Sancho ni Ronaldinho Chelsea

Muktasari:

  • Winga huyo wa Manchester United alijiunga na The Blues kwa mkopo katika siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka huu.

LONDON, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Mashabiki wa Chelsea wanaamini wamempata Ronaldinho baada ya kumwona Jadon Sancho mazoezini kwa mara ya kwanza akiwa na miamba hiyo.

Winga huyo wa Manchester United alijiunga na The Blues kwa mkopo katika siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka huu.

Sancho mambo yake hayakuwa mazuri huko Old Trafford baada ya kutibuana na kocha Erik ten Hag na sasa Chelsea imemsajili kwa mkopo wenye kipengele cha kumbeba jumla kwa Pauni 20 milioni itakapofika dirisha la usajili la majira ya kiangazi mwakani.

Sancho, 24, bado hajaanza kuichezea Chelsea, lakini mashabiki wa timu hiyo wamevutiwa baada ya kumwona akifanya mazoezi kwenye timu yao.

Winga huyo Mwingereza alionekana akifunga tu mabao kwa mpira yake aliyokuwa akipiga, tena kwenye pembe matata kabisa za magoli.

Kwa namna alivyokuwa akigonga pasi zake ziliwafanya mashabiki kumfananisha Sancho na gwiji wa Kibrazili, Ronaldinho.

Shabiki wa kwanza alisema: “Tunaye Ronaldinho wetu.” Shabiki mwingine alijibu hilo: “Atakwenda kufanya kitu kikubwa sana kwenye timu.”

Shabiki wa tatu aliongeza: “Nyakati za kuvutia. Mazoezi ya kwanza ya Jadon Cobham. Nasubiri kwa hamu kuona kile atakacholeta kwenye timu.”

Na shabiki wa nne alisema: “Bila shaka amekuja kuliamsha dude.”

Kumekuwa na matarajio makubwa kutoka kwa Sancho, lakini kitu cha kwanza ni kugombea namba kikosi cha kwanza, ambapo timu hiyo ina watu makini kama Cole Palmer na Noni Madueke. Upande mwingine wa kushoto, Sancho atagombea namba na Pedro Neto, Mykahilo Mudryk na Christopher Nkunku jambo litakalompa stresi tamu kocha Enzo Maresca.