Ulaya leo kutamu! Man U na Liverpool, Barca na Madrid, Inter na Juve

Sunday October 24 2021
ulaya pic

MANCHESTER, ENGLAND. WENGI wanasikilizia, itakuwaje huko Old Trafford - wakati ule ukuta wa Harry Maguire utakapokuwa na shughuli ya kumkabili Mohamed Salah na pacha wake, Sadio Mane na Roberto Firmino.

Hiyo ni wakati Manchester United itakapokipiga na Liverpool kwenye mchezo wa Ligi Kuu England utakaofanyika leo, Jumapili supa kabisa huko Ulaya.

Wakati kipute hicho cha mahasimu wa jadi kikisubiriwa kwa hamu huko kwenye Ligi Kuu England, Jumapili ya leo huko Ulaya kote kunawaka moto kutokana na kupigwa mechi za kibabe kabisa katika ligi kubwa.

Huko kwenye Ligue 1, Ufaransa kutakuwa na kipute matata wakati Marseille watakapokuwa nyumbani kumkaribisha Lionel Messi na jeshi lake la Neymar na Kylian Mbappe. Mechi nyingine kali kwenye Ligi Kuu Ufaransa, Nice watakuwa na kazi ya kukipiga na Lyon na AS Monaco watakipiga na Montpellier.

Moto wa Ulaya haushii hapo. Huko Italia kwenye Serie A, shughuli ni pevu wakati mabingwa Inter Milan watakapokuwa nyumbani San Siro kukipiga na Juventus. Ni mechi ya kibabe kabisa kwenye Serie A, wakati mechi nyingine itakayovutia wengi kwenye ligi hiyo itakayopigwa leo ni AS Roma ya Jose Mourinho itakapokuwa nyumbani kucheza na Napoli.

Shughuli nyingine pevu ni huko Nou Camp. Kutapigwa El Clasico ya kwanza itakayokosa makali ya Messi, wakati Barcelona itakapowakaribisha mahasimu wao wakubwa kwenye La Liga, Real Madrid kwenye mechi ya kibabe kabisa.

Advertisement

Barcelona itakuwa na matumaini makubwa kwa mastaa wake wapya akiwamo Memphis Depay na Sergio Aguero, wakati Los Blancos inaamini kwenye ubora wa wakali wake Karim Benzema, Vinicius Jr na Rodrygo - ambao wamekuwa moto kabisa kwenye kikosi hicho cha Carlo Ancelotti kwa msimu huu.

Hizo ni mechi za kibabe kabisa huko Ulaya kwa leo, huku wengi wakisubiri kuona kama Ole Gunnar Solskjaer ataepuka presha ya kufutwa kazi huko Old Trafford, huku akiwategemea mastaa wake Bruno Fernandes, Paul Pogba, Cristiano Ronaldo, Marcus Rashford na Jadon Sancho kumwokoa kwenye mtihani mzito wa kuwakabili Liverpool waliopo kwenye kiwango bora kabisa kwa sasa wakiwa hawajapoteza mechi yoyote ya ligi hadi sasa.

Mechi nyingine zitakazopigwa leo, kwenye Ligi Kuu England; Brentford watacheza na Leicester City, wakati West Ham watacheza na Tottenham Hotspur, wakati huko kwenye La Liga, Sevilla watakuwa nyumbani kucheza na Levante, Real Betis watacheza na Rayo Vallecaro na Atletico Madrid watakuwa Wanda Metropolitano kukipiga na Real Sociedad.

Kwenye Serie A, Atalanta watacheza na Udinese, Fiorentina watakipiga na Cagliari na Verona watakipiga na Lazio huku kwenye Ligue 1, Lens watacheza na Metz, Lorient watacheza na Bordeaux, Reims watacheza na Troyes na Rennes watacheza na Strasbourg, wakati kwenye Bundesliga kutakuwa na mechi tatu, FC Cologne wakicheza na Bayer Leverkusen, VfB Stuttgart watacheza na Union Berlin na Bochum watakuwa na kibarua kizito nyumbani kucheza na Eintracht Frankfurt.

Advertisement