Ukizubaa Serie A unaachwa

ROME, ITALIA. MCHAKAMCHAKA wa Ligi Kuu Italia (Serie A) umerudi na kwa leo na keshokutwa, Jumatatu, zitapigwa mechi za mzunguko wa 30 kuwania ubingwa. Hata hivyo, kinachoonekana miamba ya ligi hiyo na hasa ilizopo kwenye nafasi ya kuwania ubingwa ni kama inategeana.

Inter Milan ni kama imejitengenezea ufalme wake kwenye msimamo wa ligi na pointi 76 baada ya mechi 29, ikiziachia msala AC Milan na Juventus zilizopishana pointi tatu, ilhali Milan ikiwa nafasi ya pili na 62 na Juventus ya tatu na alama 59.

Ni hivi. Bibi Kizee cha Turin, Juventus inachofanya ni kuiombea AC Milan ipoteze dhidi ya Fiorentina na ikishinda dhidi ya Lazio na zitalingana pointi, ili ikamatie nafasi ya pili kwa tofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Hata hivyo, kwa sasa vita ni ya kumaliza nafasi ya pili licha ya zote kuwa kwenye nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Nyingine Bologna na AS Roma. Hapa kuna mtego. Kama ilivyo Juventus na AC Milan, AS Roma nayo inaombea majanga kwa Bologna itakayokutana na timu inayoburuza mkia ya Salernitana ikionekana ni maajabu kwa Bologna iliyopo nafasi ya nne kufunga na washika mkia hao walio na pointi 14.

Roma inachotaka ni kushinda mchezo wake dhidi ya Lecce na kuombea maajabu hayo ili iifikie kwa pointi Bologna (54) na kupanda kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ili kujiwekea matumaini ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Isije ikawa ni dua la kuku.

Kwingineko ni mkiani mwa msimamo huo na Sassuolo iliyopo nafasi ya 19 na pointi 23, Frosinone pointi 24, Empoli yenye pointi 25, Cagliari pointi 26 sawa na Verona zinakabana koo huku zikitegana na Frosinone inazitegea Empoli, Verona na Cagliari na moja ikipoteza  itajinusuru kwenye eneo la hatari.

Hata hivyo, ushindi kwa Frosinone utaifanya ifikishe pointi 27 na kuipita Verona iliyo nafasi ya 15 na pointi 26. Kuanzia timu inayoshika nafasi ya 18 hadi ile ya 13 yoyote itakayopoteza inaweza kujikuta ikishushwa hadi nafasi tatu za chini kwa sababu utofauti wa alama baina yao ni mbili hadi tatu.