Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pyramids, Mamelodi kumaliza ubishi fainali CAFCL

Muktasari:

  • Timu itakayopata ushindi katika mchezo wa leo itaweka rekodi ya kutwaa kombe jipya la mashindano hayo ambalo lilitambulishwa na CAF.

CAIRO, MISRI: Leo saa 2:00 usiku macho ya wapenzi wa soka barani Afrika yatakuwa kwenye Uwanja wa June 30 jijini Cairo, Misri ambapo Pyramids FC itawakaribisha Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika mechi ya marudiano ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika (CAF).

Mchezo wa kwanza ulimalizika kwa sare ya 1-1 huko Pretoria, na hivyo kufanya mechi ya leo kuwa ya kuamua bingwa wa Afrika kwa msimu wa 2024/2025.

Katika mechi hiyo, Mamelodi walikuwa wa kwanza kuandika bao la kuongoza kupitia kwa Lucas Ribeiro katika dakika ya 54, kabla ya Walid El Karti kusawazisha kwa kichwa katika dakika za majeruhi, na kuipa Pyramids faida ya bao la ugenini.

Matokeo hayo yanawapa faida kubwa wenyeji wa mchezo wa leo Pyramids kwani hata ikitokea mechi hiyo imemalizika kwa suluhu basi watakuwa mabingwa kwa faida ya kupata bao la ugenini.

Mamelodi Sundowns, maarufu kama "Masandawana", wanatafuta kutwaa taji lao la pili la CAF baada ya kulibeba kwa mara ya kwanza mwaka 2016. Wakati Pyramids wao wanalisaka taji lao la kwanza tangu kuanzishwa kwake mwaka 2008.

Kocha wa Sundowns, Miguel Cardoso, amesisitiza kuwa timu yake iko tayari kwa mchezo wa leo, licha ya faida ya bao la ugenini kwa wapinzani wao. "Tumekuwa na maandalizi mazuri na wachezaji wangu wana ari ya juu. Tunajua umuhimu wa mechi hii na tumejipanga ipasavyo," amesema Cardoso.

Kwa upande wa Pyramids FC, Kocha Krunoslav Jurcic, ameeleza matumaini ya kupata sapoti kutoka kwa mashabiki wa Misri, licha ya klabu hiyo kutokuwa na mashabiki wengi ikilinganishwa na vigogo wa Cairo, Al Ahly na Zamalek.

"Tunajua kuwa hatuna mashabiki wengi kama klabu nyingine, lakini tunatumai kuwa leo Wamisri wote watatuunga mkono kama wawakilishi wa taifa," amesema Jurcic.

Mamelodi Sundowns walifuzu katika hatua ya fainali baada ya kuiondoa Al Ahly ya Misri wakati Pyramids, waliingia fainali kwa ushindi wa jumla wa 3-2 dhidi ya Orlando Pirates na hivyo kuandika historia ya kufika fainali kwa mara ya kwanza.

Kwa kuwa sare ya 0-0 itawapa Pyramids ubingwa kwa faida ya bao la ugenini, Sundowns wanahitaji ushindi au sare ya mabao mawili au zaidi ili kutwaa taji hilo. Mechi inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, huku kila timu ikijitahidi kuandika historia mpya.