Tumerudi saiti

MUNICH, UJERUMANI. BAADA ya kusubiri kwa muda mrefu, leo pazia la michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya linafunguliwa na kutakuwa na mechi nane leo na nane kesho.

Mchezo ambao unaonekana kusubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka duniani ni ule wa Manchester United dhidi ya Bayern Munich ambao utapigwa kesho kwenye Uwanja wa Allianz Arena kuanzia saa 4:00 usiku.

Timu hizo zimekuwa na historia ya kipekee katika michuano hiyo ambapo zimekutana mara 11, huku Bayern ikiwa na rekodi nzuri zaidi mbele ya Mashetani Wekundu.

Hata hivyo, Man United imekuwa ikijivunia historia ya 1999 ambapo iliifunga Bayern kwenye mchezo wa fainali wa mashindano hayo kwa bao la jioni la OIe Gunnar Solskjaer, na baadaye ilifanikiwa kutwaa mataji matatu kwa mpigo (treble) mwaka huo.

Hata hivyo, timu hizo ambazo mara ya mwisho kukutana ilikuwa 2014, rekodi inaonyesha Man United haijawahi kupata ushindi dhidi ya Bayern tangu 2010 ambapo ilishinda mabao 3-2.

Kutokana na hali ya Man United kwa sasa katika Ligi Kuu England (EPL), watu wengi wanaipa nafasi Bayern kushinda mechi ya kesho.

Hadi sasa katika Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga), Bayern inashika nafasi ya pili ikiwa imekusanya alama 10 baada ya kucheza mechi nne, ikishinda tatu na kutoka sare moja. Wakati Man United ikiwa nafasi ya 13 kwenye msimamo wa EPL, katika mechi tano zilizopita imeshinda mbili na kufungwa tatu.

Mbali ya mechi hiyo, pia kutakuwa na mchezo mwingine mkubwa kati ya PSG na Borussia Dortmund ambao utazikutanisha mara ya kwanza kwenye historia ya timu hizo.

PSG inaingia ikiwa na kumbukumbu ya kuishia hatua ya 16 bora msimu uliopita sawa na Dortmund ambayo ilitolewa na Chelsea. PSG itakuwa nyumbani kwenye mechi hiyo.

Nayo Newcastle United ambayo inashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu kupita, ipo Italia kuvaana na AC Milan ambayo ilifika hatua ya nusu fainali msimu uliopita.

Vigogo Barcelona watakuwa nyumbani kuialika timu ya zamani ya nyota wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta, Royal Antwerp ya Ubelgiji wakati timu ya Mtanzania mwingine Novatus Dismas, Shakhtar Donetsk ya Ukraine itakuwa nyumbani kuvaana na FC Porto.

Mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Manchester City watakuwa jijini Manchester kuwaalika FK Crvena Zvezda kutoka Serbia.

Kivumbi leo.


RATIBA YA LEO

Barcelona v Royal Antwerp
(saa 4:00 usiku)
Shakhtar Donetsk v FC Porto
 (saa 4:00 usiku)
Young Boys v RB Leipzig
 (saa 1:45 usiku)
Manchester City v FK Crvena Zvezda (saa 4:00 usiku)
AC Milan v Newcastle United
(saa 1:45 usiku)
Paris Saint-Germai v Borussia Dortmund (saa 4:00 usiku)
Feyenoord v Celtic
 (saa 4:00 usiku)
Lazio v Atletico Madrid
(saa 4:00 usiku)

KESHO, JUMATANO
Benfica v FC Salzburg
(saa 4:00 usiku)
Real Sociedad v Inter Milan
 (saa 4:00 usiku)
Real Madrid v Union Berlin
 (saa 1:45 usiku)
SC Braga v Napoli
 (saa 4:00 usiku)
Arsenal v PSV Eindhoven
(saa 4:00 usiku)
Sevilla v Lens
 (saa 4:00 usiku)
Galatasaray v FC Copenhagen
 (saa 1:45 usiku)
Bayern Munich v Manchester United (saa 4:00 usiku)