Tulieni, Manchester United inambeba Kane kutuliza mashabiki

Muktasari:

OPERESHENI nyamazisha mashabiki. Mashabiki wa Manchester United wanapiga kelele nyingi kuhusu wamiliki wa klabu hiyo, familia ya Glazer kwa sasa, wakitaka waondoke kwenye timu hiyo.

LONDON, ENGLAND. OPERESHENI nyamazisha mashabiki. Mashabiki wa Manchester United wanapiga kelele nyingi kuhusu wamiliki wa klabu hiyo, familia ya Glazer kwa sasa, wakitaka waondoke kwenye timu hiyo.

Maandamano makubwa yalifanyika Jumapili iliyopita, kiasi cha kusababisha mechi ya Ligi Kuu England baina ya Man United na mahasimu wao, Liverpool, iliyopangwa kufanyika Old Trafford kuahirishwa. Shida ya mashabiki ni familia ya Glazer iondoke kwenye timu hiyo.

Lakini, sasa familia hiyo ya Kimarekani imekuja na mpango wa kuwanyamazisha mashabiki hao kwa kuwaletea kwenye kikosi mastaa wanaowataka ili wawekeze nguvu kwenye kushangilia timu - kwa maana ya kupata burudani ya kutosha ndani ya uwanja na kuondoa pingamizi zao dhidi ya wamiliki.

Na sasa familia hiyo ya Glazer ipo tayari kutumia Pauni 90 milioni kunasa huduma ya straika wa Tottenham Hotspur, Harry Kane kuhakikisha anakuja kukipiga Man United msimu ujao na kuwanyamazisha kabisa mashabiki.

Maandamano ya Jumapili yametuma ujumbe mkubwa Florida, mahali ambako familia hiyo ya Glazer inaishi na sasa wanataka kumaliza hasira za mashabiki kwa kuwatelea straika matata kabisa kwenye Ligi Kuu England akaongoze safu ya ushambuliaji ya miamba hiyo ya Old Trafford.

Wamiliki hao wa Man United hawana mpango wa kuiuza timu yao na badala yake wanataka kurudisha mapenzi ya mashabiki kwa kuwaletea mastaa wanaowataka na wataanzia na straika Kane.

Kitu cha kwanza kwenye mpango woa ni kujaribu kusajili straika wa kiwango cha dunia, ambaye kocha Ole Gunnar Solskjaer anamtaka.

Straika wa Spurs, Kane yupo kwenye rada zao na kinachoripotiwa ni kwamba mshambuliaji huyo Mwingereza naye anavutiwa na mpango wa kwenda kukipiga Old Trafford.

Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy amekuwa akidai kwamba hata kama ataamua kumuuza Kane, basi hatafanya hivyo kwa klabu ya Ligi Kuu England. Lakini, klabu hiyo ya London itahitaji pesa kwa ajili ya kuboresha kikosi chake, hivyo kugomea ofa kama hiyo tamu kabisa itakuwa kitu kigumu.

Na mabosi wa Man United wamepanga kumjaribu Levy kwa mkwanja wa Pauni 90 milioni kwenye ofa yao ya kuanzia kwa Kane, 27, huku fowadi huyo akiwa na mpango wa kuondoka ili akajiunge na timu itakayompa nafasi ya kunyakua mataji.

Kane, ambaye amefunga mabao 31 na kuasisti mara 16 msimu huu, alifichua mwezi Machi, mwaka huu kwamba, anataka timu itakayokuwa na ushindani ndani ya uwanja ili kufukuzia mataji.

Akizungumza wakati alipokabidhiwa tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu wa Ligi Kuu England ka London katika sherehe za London Football Awards, Kane alisema: “Unapotazama nyuma mwishoni mwa maisha yako ya soka, haya ni mambo utakayokuwa unayatazama kwa ukubwa na lengo la sasa ni kuwa mchezaji wa kuipa timu mataji.

“Kama ilivyo kwa ukubwa wa jambo hili, nataka kushinda kitu kikubwa kabisa nikiwa na timu. Kwa sasa tunashindwa kufanya hivyo. Inaumiza, lakini ndivyo ilivyo. Nafurahi nimeshinda tuzo hii ya mchezaji bora wa mwaka wa Ligi Kuu na hakika umekuwa msimu wangu mzuri ndani ya uwanja.”

Bosi wa Spurs, Levy anamthaminisha Kane kuwa na thamani ya Pauni 170 milioni, lakini uhalisia ni kwamba hana thamani hiyo tangu kuibuka kwa janga la corona.

Na familia ya Glazer kwa sasa haina ujanja zaidi ya kufungua tu pochi kuwapoza mashabiki wa Man United wasiendelee na vurugu zao kwa sababu wanaamini kila kitu kitakwisha timu ikianza kubeba mataji hasa ya Ligi Kuu England.

Hata hivyo, jambo hilo pengine linaweza lisiwapoze mashabiki, lakini litawafurahisha wawekezaji ambao wamekuwa wakitoa pesa zao kuidhamini timu hiyo kuona inafanya kweli ndani ya uwanja na kujiongezea umaarufu.