Tudor akiri mambo magumu Spurs
Muktasari:
- Kocha huyo raia wa Croatia alikuwa akisimamia mechi yake ya nne tu akiwa kwenye benchi la Spurs wakati timu yake ilisafiri kwenda kucheza dhidi ya miamba ya Hispania, Jumanne.
LONDON, ENGLAND: KOCHA Igor Tudor amekiri kuwa mambo yote yanaonekana kwenda vibaya Tottenham Hotspur huku shinikizo likiongezeka juu ya nafasi yake baada ya aibu waliyoipata katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mbele ya Atletico Madrid, usiku wa Jumanne.
Kocha huyo raia wa Croatia alikuwa akisimamia mechi yake ya nne tu akiwa kwenye benchi la Spurs wakati timu yake ilisafiri kwenda kucheza dhidi ya miamba ya Hispania, Jumanne.
Tudor alishuhudia kipigo cha mabao 5-2 kutoka kwa Atlético Madrid, ambapo makosa matatu makubwa ya safu ya ulinzi yalichangia sana matokeo hayo. Matumaini yoyote ya kupata ushindi wa kwanza au hata kuepuka kushindwa kwa mara ya kwanza chini yake, yalizimwa haraka baada ya wenyeji kufunga mabao manne ndani ya dakika 25 za mwanzo.
Makosa ya kuteleza kutoka kwa kipa wa akiba Antonín Kinský pamoja na beki Micky van de Ven yaliipa Atlético nafasi ya kupata uongozi wa mapema. Kisha jaribio baya la pasi kutoka kwa Kinský liliongeza matatizo zaidi pale alipomruhusu Julian Alvarez kufunga kirahisi kwenye lango tupu. Kipa huyo wa Czech mwenye miaka 22 alitolewa uwanjani dakika moja baadaye na Tudor.
Lakini, hiyo haitoshi kuonyesha matatizo ya Spurs msimu huu, kipa aliyeingia kuchukua nafasi yake Guglielmo Vicario karibu mara moja aliruhusu bao la nne lililofungwa na Robin Le Normand. Tudor aliyeshangaa hakuweza kufanya mengi zaidi ya kuomba radhi kwa mashabiki waliokuwa wamesafiri kufuatilia timu yao, licha ya mabao mawili yaliyofungwa na Pedro Porro na Dominic Solanke kupunguza tofauti hadi mabao matatu kabla ya kurejea Kaskazini mwa London.
Akizungumza na TNT Sports, Tudor alisema: “Ulikuwa mchezo wa ajabu. Tuliwapa mabao matatu. Tulianza vizuri tena, lakini matatizo yakatuua. Ni jambo la ajabu sana na lisilo la kawaida. Hilo lilipunguza kujiamini kwetu.”
Aliongeza: “Tunawaomba radhi mashabiki waliokuwa hapa leo na kila mtu kwa ujumla. Wamepitia wakati mgumu.”