Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mechi 34 bila kupoteza zaipa mwanga mpya Morocco

KUPOTEZA Pict

Muktasari:

  • Timu hiyo ya Afrika Kaskazini haikuonyesha mchezo wa kupendeza ilipoiondoa Canada, mmoja wa waandaaji wa Kombe la Dunia 2026, katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa Houston, Marekani.

TEXAS, MAREKANI: MOROCCO inaendelea kuandika historia nyingine katika Kombe la Dunia, ingawa ushindi wao wa mabao 3-0 dhidi ya Canada haukuwa wa soka la kuvutia bali ulikuwa wa nidhamu, uimara na ufanisi.

Timu hiyo ya Afrika Kaskazini haikuonyesha mchezo wa kupendeza ilipoiondoa Canada, mmoja wa waandaaji wa Kombe la Dunia 2026, katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa Houston, Marekani.

Cha kushangaza ni kwamba Morocco ilishinda licha ya kupiga mashuti matano pekee yaliyolenga lango, idadi ndogo zaidi kuwahi kurekodiwa kwa timu iliyoshinda mechi ya hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia. Aidha, kipindi cha kwanza kilivunja rekodi kwa kuwa na kadi nyingi za njano kuliko idadi ya mashuti.

Hata hivyo, Morocco ilifanikiwa kuvuka salama. Kama msemo wa soka unavyosema, timu kubwa hujua kushinda hata inapocheza vibaya.

Kwa sasa hakuna shaka kuwa Morocco ni timu kubwa na miongoni mwa wagombea halisi wa kutwaa Kombe la Dunia.

Siyo tu kwamba haijapoteza mchezo wowote katika mashindano haya, bali pia haijafungwa katika mechi zake 34 zilizopita kwenye mashindano yote.

KUPO 01

Ingawa rekodi hiyo ina mjadala kwa sababu inahusisha fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2026 dhidi ya Senegal, ambapo ushindi ulitunukiwa Morocco baadaye na bado unapingwa mahakamani, bado ni rekodi ya kuvutia.

Mara ya mwisho Morocco ilipoteza mchezo Agosti 2025 ilipofungwa 1-0 na Kenya katika Mashindano ya CHAN, yanayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani pekee.

Baada ya dakika 15 za mwanzo dhidi ya Canada nchini Marekani, Morocco haikuonekana tena kuwa katika hatari ya kupoteza mchezo.

Canada ilipata nafasi mbili za mapema kupitia Jonathan David na Tani Oluwaseyi, lakini kipa Yassine Bounou aliokoa hatari zote. Wakati huo huo, Morocco haikugusa mpira ndani ya eneo la hatari la wapinzani kwa dakika 15 za kwanza, jambo lililotokea pia katika mchezo wao uliopita.

KUPO 02

Lakini walipoanza kuzoea mchezo, walidhibiti kila kitu. Kocha wa Canada, Jesse Marsch, amesema baada ya mechi: "Walionekana kuyumba kidogo, lakini hawakuvunjika."

Katika pambano hilo lililozikutanisha timu mbili zenye kizazi bora cha wachezaji, Morocco ndiyo iliyoangaza zaidi.

Kwa upande wa Canada, Alphonso Davies aliyekuwa majeruhi aliangalia kutoka benchi huku Morocco ikimdhibiti Stephen Eustaquio na kumzuia kabisa mshambuliaji Jonathan David.

Nahodha Achraf Hakimi aliendelea kuthibitisha ubora wake kama mmoja wa mabeki bora wa kulia duniani, akitoa mchango mkubwa katika safu ya ushambuliaji na ulinzi. Kiungo mshambuliaji Brahim Diaz alitoa pasi mbili za mabao na sasa ana jumla ya pasi nne za mabao katika historia ya Kombe la Dunia, nyingi zaidi kuwahi kufanywa na mchezaji wa Afrika.

KUPO 03

Kocha wa Morocco, Mohamed Ouahbi, amesema: "Kipindi cha kwanza kilikuwa kigumu sana. Tulifanya marekebisho wakati wa mapumziko. Hatukuwahi kuhisi tuko salama dhidi ya presha yao."

Aliongeza: "Hatukubadili utambulisho wetu wala falsafa yetu ya mchezo. Katika Kombe la Dunia lazima ukutane na nyakati ngumu. Muhimu ni kuwa imara hata usipokuwa katika kiwango chako bora, na kukumbuka unamchezea nani na unachezea nini."

Ushindi huo umeipeleka Morocco robo fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya pili mfululizo baada ya mafanikio ya Qatar 2022.

Sasa Morocco imeshinda mechi nne za hatua ya mtoano katika historia ya Kombe la Dunia, mbili mwaka 2022 na mbili mwaka 2026, idadi inayolingana na ushindi wa mataifa yote mengine ya Afrika kwa pamoja.

KUPO 04

Ikishinda mchezo mmoja zaidi, italinganisha mafanikio yake ya mwaka 2022 ilipokuwa taifa la kwanza la Afrika kufika hatua ya nusu fainali.

Hata hivyo, bado kuna wanaoamini Morocco haijakutana na mtihani mgumu zaidi.

Iliianza michuano kwa sare ya 1-1 dhidi ya Brazil, ikaifunga Scotland kwa tabu bao 1-0, kisha ikaifunga Haiti 4-2, hii yote ni hatua ya makundi. Katika hatua ya 32 bora iliiondoa Uholanzi kwa penalti 3-2, kabla ya kuifunga Canada kwa mabao 3-0 hatua ya 16 bora.

KUPO 05

Mchambuzi wa BBC Radio 5 Live, Chris Sutton, amesema: "Morocco haikuwa katika kiwango chake bora, na mitihani migumu zaidi bado ipo. Walionekana wazito mwanzoni mwa mchezo. Labda waliidharau Canada."

Aliongeza: "Kadri mchezo ulivyoendelea walizidi kuwa imara. Wao ni hatari sana kwenye mashambulizi ya kushtukiza. Lakini kama watacheza dhidi ya Ufaransa kwa kiwango walichoonyesha kipindi cha kwanza, wanaweza kuadhibiwa vibaya."

Hata hivyo, hakuna shaka kuwa Morocco ndiyo taifa la Afrika lenye nafasi kubwa zaidi kuwahi kutwaa Kombe la Dunia.

Mafanikio ya Morocco hayakuja kwa bahati. Yamejengwa juu ya uwekezaji wa muda mrefu uliofanywa kwa msaada wa Mfalme Mohammed VI.

KUPO 06

Chuo cha kukuza vipaji pamoja na kituo cha kisasa cha mazoezi chenye thamani ya dola milioni 65, vyote vikibeba jina lake, vilifunguliwa mwaka 2009 na 2019. Miundombinu hiyo imeisaidia Morocco kuwa taifa lenye nafasi ya juu zaidi Afrika katika viwango vya FIFA.

Ouahbi amesema: "Kila kinachotokea leo katika soka la Morocco ni kutokana na Mohammed VI. Amewekeza sana, hasa katika akademi hii."

Baada ya kufuzu Kombe la Dunia mara tatu kati ya 1986 na 1998, Morocco ilikosa mashindano hayo kwa miaka 20 mfululizo.

Uwekezaji huo uliifanya iweze kurejesha mafanikio na kuwavuta wachezaji wenye asili ya Morocco waliokulia nje ya nchi kama Achraf Hakimi na Brahim Diaz, ambao wote walizaliwa Hispania.

Leo Morocco imejijengea uwezo mkubwa wa ushindani na kujiamini, jambo ambalo limekuwa mfano kwa mataifa mengine ya Afrika na Kiarabu.

Ouahbi amesema: "Sasa sisi si timu ya kushangaza tena. Watu wanapoitaja Morocco wanazungumzia mgombea halisi wa ubingwa na taifa kubwa la soka. Hilo linatupa fahari kubwa."

Alimalizia kwa kusema: "Huu ni mwanzo tu. Tunataka kuendelea kufanya vizuri katika Kombe la Dunia kwa miaka mingi ijayo. Hatutaki kusimama."

Tofauti na safari yao ya Qatar 2022 iliyokuwa ya kushangaza wengi, safari ya Morocco katika Kombe la Dunia 2026 imejaa malengo makubwa na imani kwamba wanaweza kufika kileleni.