Trump atunukiwa Tuzo ya Amani ya FIFA
Muktasari:
- Tuzo hiyo imeanzishwa mwaka huu na Rais wa Fifa, Gianni Infantino, na hutolewa kwa mtu ambaye amechukua hatua za kipekee na za kiubunifu kwa ajili ya amani na kuiunganisha dunia.
Rais wa Marekani, Donald Trump, amepokea Tuzo ya Amani ya FIFA ya kwanza kabla ya droo ya Kombe la Dunia la Fifa 2026 iliyofanyika Desemba 5, 2025 huko Washington, Marekani.
Tuzo hiyo imeanzishwa mwaka huu na Rais wa Fifa, Gianni Infantino, na hutolewa kwa mtu ambaye amechukua hatua za kipekee na za kiubunifu kwa ajili ya amani na kuiunganisha dunia.
Ilitarajiwa Trump ambaye aliwasili kwenye hafla hiyo pamoja na Infantino na kufanya naye maonyesho kadhaa ya hadharani katika miezi ya hivi karibuni, angeibuka mshindi.
Mbali na kupokea kombe kubwa la dhahabu, Trump pia alikabidhiwa medali na cheti na Infantino kabla ya kutoa hotuba.
Trump amedai kuwa ameokoa mamilioni ya watu kupitia hatua mbalimbali za kidiplomasia na kwamba amesitisha vita kabla havijaanza.
“Hii ni moja ya heshima kubwa sana katika maisha yangu,” Trump amesema, kabla ya kudai kwamba Kombe la Dunia la 2026 limeweka rekodi mpya ya mauzo ya tiketi.
“Gianni amefanya kazi ya ajabu. Hii ni heshima nzuri kwako na mchezo wa mpira wa miguu au tunavyouita hapa soka. Mauzo yako juu zaidi ya tulivyotarajia,” Trump amesema.
“Dunia sasa ni mahali salama zaidi. Marekani haikuwa katika hali nzuri mwaka mmoja uliopita, sasa sisi ndiyo nchi inayovutia zaidi duniani.”
Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitafanyika kwa ushirikiano wa nchi za Marekani, Canada na Mexico, kuanzia Juni 11, 2026 hadi Julai 19, 2026.
Baadaye, Trump alirudi jukwaani pamoja na Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum, na Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, kufanya ufunguzi wa droo hiyo.
Viongozi hao watatu walitoa mipira ya nchi zao, zilizokwishapangiwa makundi yao. Baada ya hapo, wote watatu walipiga selfie iliyochukuliwa na Infantino.
Mexico wapo Kundi A na watacheza mechi ya ufunguzi. Canada wapo Kundi B na Marekani ipo Kundi D.
Trump, baada ya kurudia kauli zake kuhusu mauzo ya tiketi, alitania kuhusu mgongano wa majina kati ya American Football na kile ambacho Wamarekani wengi hukiita Soccer.
“Tunahitaji kulitafutia jina jingine NFL,” Trump amesema.
“Huu hapa ndiyo mpira wa miguu, tunaouita soccer Marekani, lakini kwa kweli ni mpira wa miguu. Haieleweki kwamba tunauita soccer.”