Messi aibeba Argentina, yatinga robo fainali dakika za jioni
Muktasari:
- Misri ilionekana kuwa njiani kuandika historia kubwa baada ya kuongoza kwa mabao mawili lakini ubora wa nahodha, Lionel Messi uliigeuza kabisa mechi hiyo katika dakika za mwisho na kuiwezesha Argentina kuendelea na safari ya kutetea ubingwa wake.
BINGWA mtetezi wa Kombe la Dunia, Argentina, imeonyesha kwa mara nyingine kuwa ni moja ya timu hatari zaidi duniani baada ya kutoka nyuma kwa mabao mawili na kuibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya Misri katika mchezo wa hatua ya 16 bora na kufuzu robo fainali.
Misri ilionekana kuwa njiani kuandika historia kubwa baada ya kuongoza kwa mabao mawili lakini ubora wa nahodha, Lionel Messi uliigeuza kabisa mechi hiyo katika dakika za mwisho na kuiwezesha Argentina kuendelea na safari ya kutetea ubingwa wake.
Misri ilianza mchezo kwa ujasiri na kufungua ukurasa wa mabao dakika ya 15 kupitia Yasser Ibrahim, aliyefunga kwa kichwa baada ya mpira wa krosi.
Argentina ilipata nafasi ya kusawazisha dakika chache baadaye baada ya kupewa penalti kufuatia kosa la Haissem Hassan, lakini Messi alishindwa kuitumia baada ya kipa Mostafa Shobeir kuokoa mkwaju huo na kuendeleza kiwango chake bora katika michuano hiyo.
Baada ya penalti hiyo, Argentina iliongeza mashambulizi huku Alexis Mac Allister, Julián Alvarez na Messi wakikosa nafasi kadhaa kutokana na ubora wa Shobeir, ambaye aliendelea kuwa mwiba kwa washambuliaji wa La Albiceleste kipindi chote cha kwanza.
Kipindi cha pili kilianza kwa Argentina kuendelea kulisakama lango la Misri lakini ilikaribia kuadhibiwa zaidi baada ya Mostafa Ziko kufunga bao ambalo baadaye lilibatilishwa na VAR kutokana na faulo katika mwanzo wa shambulizi.
Hata hivyo, onyo hilo halikutosha kwa Argentina kwani dakika chache baadaye Misri ilipata bao la pili.
Safari hii Mohamed Salah alionyesha ubora wake kwa kutoa pasi nzuri iliyomkuta Hassan ambaye alitengeneza nafasi kwa Mostafa Ziko kufunga na kuiweka Misri mbele kwa mabao 2-0.
Wakati wengi wakiamini mchezo ulikuwa umekwisha, Argentina ilianza kurejea taratibu.
Dakika ya 79, Cristian Romero aliifungia Argentina bao la kwanza kwa kichwa akimalizia krosi maridadi ya Messi na kuamsha matumaini ya mabingwa hao.
Dakika chache baadaye Messi aliisawazishia Argentina kwa shuti kali lililomshinda Shobeir, akiendeleza rekodi yake ya kufunga katika mechi tisa mfululizo za Kombe la Dunia. Tayari amefikisha mabao manane akiwa kinara wa ufungaji katika michuano ya mwaka huu.
Mchezo ulipoingia muda wa nyongeza, timu zote zilishambulia kwa kasi huku Misri ikidai penalti ambayo haikutolewa.
Argentina ilitumia mwanya huo kufanya shambulizi la kushtukiza ambapo Lautaro Martínez alipenya upande wa kulia na kutoa krosi safi iliyomaliziwa kwa kichwa na Enzo Fernández, aliyefunga bao la ushindi lililoivusha Argentina kwa ushindi wa mabao 3-2.
Messi alikuwa nyota wa mchezo huo kwa kutoa pasi ya bao moja, kufunga bao la kusawazisha na kuiongoza timu kurejea kutoka katika hali ngumu, hali iliyomfanya kutangazwa kuwa Mchezaji Bora.
Kwa ushindi huo, Argentina imefuzu robo fainali na sasa itakutana na mshindi kati ya Uswisi na Colombia, huku ikiendelea kuota ndoto za kuwa timu ya kwanza tangu Brazil mwaka 1962 kutetea kwa mafanikio taji la Kombe la Dunia.
Kwa upande wa Misri, itaondoka na maumivu makubwa baada ya kushindwa kulinda uongozi wa mabao mawili katika dakika za mwisho, licha ya kuonyesha kiwango bora kwa sehemu kubwa ya mchezo.