Timu hizi zilishtua UEFA

LONDON, ENGLAND. MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa kwa hatua ya makundi rasmi ilianza wiki hii na timu 32 zilishuka dimbani kuanza kampeni za kufuzu hatua ya 16 bora.
Wakati michuano hii ikiendelea moja kati ya vitu ambavyo huzuka mara kwa mara huwa ni kufanya vizuri kwa timu ambazo hazikuwa zinapewa nafasi kubwa.
Kwenye michiano ya mwaka huu pia mambo yanaonekana kuwa huenda yakawa hivyo kwani Newcastle imefanikiwa kuchukua pointi kwa AC Milan ambayo ilifika nusu fainali kwa msimu uliopita. Hapa tumekuletea timu tano zilizowahi kutikisa na kuchukua ubingwa licha ya kutopewa nafasi hiyo wakati michuano inaanza na msimu huu mambo yanaweza yakawa hivyo pia.
5. Inter Milan (2009-10)
Ilimaliza nafasi ya pili nyuma ya Barcelona kwenye hatua ya makundi, halafu katika 16 bora ikacheza dhidi ya Chelsea na kuitoa kwa tofauti ya mabao 2-1, kisha robo fainali ikaifunga CSKA Moscow kwa jumla ya mabao 2-0.
Kazi ilikuwa kwenye hatua ya nusu fainali ambapo ilicheza na Barcelona iliyokuwa ya moto kwa wakati huo na ndio ilikuwa bingwa mtetezi na mbaya zaidi kwenye hatua ya makundi Inter ilipoteza mabao 2-0 mbele yao.
Hata hivyo, kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza Inter ilishinda mabao 3-1, lakini bado watu wengi waliamini safari ya timu hiyo kutoka Italia itaenda kuishia Nou Camp.
Mechi ya mkondo wa pili mambo yakawa tofauti kwa Barca ambayo ilipata bao moja tu na kuipa Inter nafasi ya kusonga kwa jumla ya mabao 3-1 na hiyo ilitokana na jinsi Mourinho alivyoingia kwa mbinu ya kupaki basi. Fainali ikacheza na Bayern Munich iliyokuwa chini ya Louis Van Gaal na ikashinda 2-0, yaliyofungwa na Eder Militao.
4. Liverpool (2004-05)
Mechi ya fainali ya mwaka huu imepewa jina la maajabu ya Istanbul. Liverpool ilifungwa mabao matatu katika kipindi cha kwanza na ikayarudisha yote kipindi cha pili na kwenda kuchukua ubingwa kwa penalti mbele ya AC Milan.
Ili kufuzu michuano hiyo Liverpool ilimaliza nafasi yanne katika Ligi Kuu England ikiwa na alama 15 tofauti kati mbele ya Man United iliyomaliza nafasi ya tatu.
Kutokana na kiwango chao mashabiki hawafikiria kama ingepata taji hilo chini ya Rafa Benitez, Liverpool ilizitoa Bayern Munich, Juventus na Chelsea kwenye hatua za mtoano kisha ikacheza fainali na AC Milan.
3. Porto (2003-04)
Jose Mourinho alijitangaza kama mmoja kati ya makocha bora duniani baada ya kushinda taji hili la Ligi ya Mabingwa akiwa na timu ambayo haikupewa nafasi kabisa.
Wakati Mourinho anaichukua Porto hakukuwa na uwezekezaji wa kutosha ambao ungewawezesha kusajili wachezaji bora kutoka timu mbalimbali barani Ulaya lakini kupitia mbinu zake na wachezaji wasiokuwa na uzoefu alishinda taji.
Watu walishangazwa na timu hii baada ya kuindoa Man United kwenye hatua ya 16 bora na Olympique Lyon kwenye ya robo fainali.
Kwenye hatua ya nusu fainali ilikutana na Deportivo La Coruna, mechi ya marudiano ilikuwa ngumu sana lakini Porto iliingia fainali kwa bao moja ililoshinda nyumbani na mchezo wa fainali ikaifunga Monaco 3-0.
2. Chelsea (2011-12)
Mambo hayakuwa mazuri kwa Chelsea msimu huu na zaidi kwenye Ligi Kuu England, ilimfukuza kocha wake Andre-Vilas Boas na nafasi yake ikachukuliwa na Roberto di Matteo aliyekuwa anahudumu kama kocha wa muda.
Katika hali isiyo ya kawaida Chelsea ilifanikiwa kuchukua ubingwa wa Ulaya, ilishafungwa mabao 3- 1 ugenini, hatua ya 16 bora dhidi ya Napoli ikaenda kupindua meza kibabe nyumbani kwa kushinda mabai 4-1 na kupenya hatua ya robo fainali ilikutana na Benfica ambayo iliifunga mechi zote mbili. Nusu fainali ikakutana na Barcelona ambayo iliifunga bao 1-0 pale Stamford Bridge na baadaye ikapata sare pale
Nou Camp na fainali na Bayern Munich ikachukua taji. Msimu huu ilimaliza nafasi ya sita kwenye EPL.
1. BorussiaDortmund (1996/97)
Kipindi hiki Borussia Dortmund ilikuwa na kiwango bora Ligi Kuu Ujerumani lakini haikupewa nafasi ya kuchukua taji la Ligi ya Mabingwa.
Kwenye mechi ya fainali ilicheza dhidi ya Juventus ndio ilionekana kuwa safari yake imefika mwisho. Juve ya wakati huo ilikuwa na mastaa kama Deschamps, Zidane, Vieri na Del Piero, Lakini ilishinda 3-1 na kutwaa ubingwa. Kwenye makundi pia ilimaliza nafasi ya pili nyuma ya Atletico Madrid, robo ikaitoa Auxerre ya Ufaransa na nusu fainali iliitoa Man United na Sir Alex Ferguson ambayo ilisheheni mastaa kibao.