Thubutu! Vigogo Liverpool waghairi kuondoka

New Content Item (1)
New Content Item (1)

LIVERPOOOL, ENGLAND. MABOSI wa Liverpool wamebadili uamuzi wao wa kuiuza timu hiyo na kuondoka jumla badala yake wanafikiria kuuza sehemu ndogo tu ya hisa na kuendelea kuwa wamiliki wakuu wa timu hiyo.

Liverpool ambayo inamilikiwa na Fenway Sports Group iliwekwa sokoni Novemba mwaka jana ikisubiria dau kubwa lakini hadi sasa wamiliki bado hawajapata ofa nzuri wanayohitaji.

Vigogo hao walikuwa wakihitaji kiasi kisichopungua Pauni 4 bilioni ili kuiuza timu hiyo lakini ofa ambazo zimefika mezani hadi sasa hazijafikia kwenye kiasi hicho cha pesa.

Mchakato mzima wa kuuzwa kwa timu unasimamiwa na kampuni za Goldman Sachs na Morgan Stanley ambazo zimefanya kazi kubwa kuhakikisha zinatafuta watu watakaokuwa tayari kuweka pesa mezani.

Inadaiwa watu wote hao wanaotaka kuinunua timu hiyo wameweka mezani kati ya Pauni 3 bilioni na Pauni 3.5 bilioni ambazo hazijaonekana kuwashawishi wamiliki.

Asilimia kubwa ya ofa hizo zimeripotiwa kutokea kwa matajiri wa Kimarekani kwani wawakilishi wa kampuni hizo wamewahi kuonekana nchini England kwa kile kinachoelezwa kwamba waliwasili kwa ajili ya kufanya mazungumzo.

Miongoni mwao ni mmiliki wa timu ya mpira wa kikapu ya LA Clippers, Steve Ballmer, mmiliki wa Boston Celtics, Steve Pagliuca sambamba na familia ya The Ricketts.
Awali, kulikuwa na ripoti zinazodai kwamba kampuni kadhaa kutoka uarabuni na mashariki ya kati kama DIC (Dubai International Capital) zimeonyesha nia ya kutaka kuinunua timu hiyo lakini taarifa hiyo ilikanushwa.
FSG iliinunua Liverpool kwa Pauni 300 milioni kutoka kwa Tom Hicks na George Gillett mwaka 2010 na imeiwezesha kuwa moja kati ya timu tishio duniani katika miaka ya hivi karibuni kwa kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya 2019 na lile la Ligi Kuu

England ililotwaa baada ya kulikosa kwa miaka 30.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka tovuti ya The Athletic ni kwamba mabosi wa Liverpool wamebadilisha msimamo wao na wanataka kuendelea kukaa kwenye timu kama wamiliki wenye hisa nyingi zaidi hata kama watauza baadhi ya hisa.

Liverpool imekuwa kwenye hali mbaya kwa msimu huu ikishika nafasi ya tisa hadi sasa baada ya kucheza mechi 18 na kukusanya alama 28, hali inayotishia uwepo wao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kwa msimu ujao.

Kwa msimu uliopita timu hii imeripotiwa kukusanya mapato ya Pauni 600 milioni kiasi ambacho ni mara tano ya hiyo pesa iliyowekwa mezani na kampuni na watu wanaotaka kuinunua.
Hii ni moja ya sababu ambazo zimewafanya vigogo hawa waamue kubadili uamuzi wa kuuza hisa nyingi na badala yake waendelee kukaa ili wapige pesa.

Kwa mara ya kwanza licha ya kukubali kuiuza, hawakuwa wanataka kuuza hisa zote, walitaka kuuza hisa nyingi na wao kubakiwa na asilimia chache lakini raundi hii watauza chache kisha wabakiwe na nyingi.

Taarifa zinaeleza kuwa mabosi hao wameamua kuuza baadhi ya hisa za timu baada ya kufeli kwa mpango wao wa European Super League ambapo Aprili,  2021, matajiri hao waliungana vigogo wengine barani Ulaya na kuweka wazi kwamba walitaka kuanzisha michuano yao binafsi mbali ya ile ya UEFA, lakini ilishindikana baada ya mashabiki wa soka Ulaya nzima kugoma.