Thierry Mouyouma: Gabon imeadhibiwa kwa makosa yetu
Muktasari:
- Kocha Mouyouma, amesema timu ilionyesha uwezo mkubwa wa kupambana katika sehemu kubwa ya mchezo huo, lakini baadhi ya makosa madogo madogo hasa katika muda wa nyongeza, yaliwagharimu na kutoa nafasi kwa Nigeria kupata mabao matatu.
Kocha wa timu ya taifa ya Gabon, Thierry Mouyouma, amefichua makosa yaliyoiponza ipoteza mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia 2026, mbele ya Nigeria iliyochomoz ana ushindi 4-1, jana Alhamisi, Novemba 13.
Kocha Mouyouma, amesema timu ilionyesha uwezo mkubwa wa kupambana katika sehemu kubwa ya mchezo huo, lakini baadhi ya makosa madogo madogo hasa katika muda wa nyongeza, yaliwagharimu na kutoa nafasi kwa Nigeria kupata mabao matatu.
Amesema pamoja na udhaifu huo, picha wachezaji hawakuwa makini kila walipofika eneo la hatari za mpinzani, hali ambayo amekiri imewanyima nafasi ya kufikia lengo walilokuwa wamejiwekea katika mechi hiyo muhimu.
“Hatukuwa wazuri katika eneo la mpinzani, hatukulinda vizuri kwenye eneo letu. Nigeria ilifanya yote na kufunga,” Mouyouma amesema ma kuongeza;
“Mechi ilikuwa 50 kwa 50 ndani ya dakika 90, lakini mambo yalitugeukia baada ya dakika 30 kuongezwa, hapa wachezaji wangu alionyesha udhaifu mkubwa sana na kutoa nafasi kwa wapinzani wetu kutufunga mabao matatu na mwisho wa mechi tukapoteza kwa 4-1.”
Licha ya kuumizwa na matokeo ya mechi hiyo, Mouyouma amesisitiza, uzoefu walioupata kupitia mechi hiyo utawasaidia katika michuano mingine siku za usoni, hasa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON).
“Tumepata funzo kubwa na tunalichukuwa kuelekea AFCON 2025. Matokeo haya yametuumiza, lakini hatuna budi kuyabeba kama chachu ya kusaka mafanikio zaidi kwa siku za usoni,” amesema.
Gabon ilikuwa Kundi F katika mchujo wa Kombe la Dunia 2026 kwa bara la Afrika. Wakati wa mchujo huo, timu hiyo ilionyesha umahiri mkubwa na kushinda mechi kadhaa muhimu ambazo ziliwapa nafasi ya kucheza mechi ya mchujo dhidi ya Nigeria.
Gabon ilipata ushindi 4-0 dhidi ya Shelsheli, ambapo Denis Bouanga alifunga hat-trick, kisha 2-1 dhidi ya Kenya, mabao yakiyofungwa na Pierre-Emerick Aubameyang. Pia, katika mechi nyingine yenye ushindani mkubwa dhidi ya Gambia, Gabon ilishinda 4–3 huku Aubameyang akifunga tena mabao muhimu.
Mafanikio haya katika mchujo wa kundi, pamoja na pointi ilizokusanya, yaliipa Gabon nafasi ya kucheza mechi ya mchujo wa nusu fainali dhidi ya Nigeria, hatua ambayo ilikuwa muhimu katika ndoto ya taifa hilo la Afrika Magharibi kufuzu Kombe la Dunia 2026.