Chelle aipongeza Super Eagles, afichua siri ya ushindi
Muktasari:
- Chelle amewapongeza wachezaji kwa juhudi na kupambana wakati wote, hali ambayo anaamini ilichagiza kupatikana kwa matokeo hayo, yanayoipeleka Nigeria katika mechi ya fainali ya mchujo ya Kombe la Dunia 2026.
Kocha mkuu wa Super Eagles, Eric Chelle, ameshindwa kuficha furaha yake baada ya ushindi wa mkubwa wa 4–1 dhidi ya Gabon katika mechi ya nusu fainali ya mchujo wa Kombe la Dunia 2026, iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Prince Moulay El Hassan mjini Rabat, Morocco.
Chelle amewapongeza wachezaji kwa juhudi na kupambana wakati wote, hali ambayo anaamini ilichagiza kupatikana kwa matokeo hayo, yanayoipeleka Nigeria katika mechi ya fainali ya mchujo ya Kombe la Dunia 2026.
“Ninajivunia sana wachezaji wangu, kwa sababu kila wakati wanazingatia kile nilichowaomba wakifanye, nilikichotaka, na walionyesha kile nilichokitarajia. Neno kuu kwenye mechi ya jana lilikuwa hamasa. Wakati wa hotuba yangu lilikuwa kuhusu hamasa, kufanya kazi pamoja ili kufikia kitu kimoja,” amesema Chelle.
Katika mechi hiyo, mshambuliaji wa Sevilla, Akor Adams, aliwaweka Super Eagles kifua mbele zikiwa zimesalia dakika 12 kabla dakika 90 kukamilika, huku Panthers ikirejea mchezoni baada ya kiungo Mario Lemina kusawazisha katika dakika ya 88.
Nigeria ilipata bao la pili kupitia mchezaji wa akiba Chidera Ejuke katika dakika ya 97. Victor Osimhen alifunga mabao mawili na kukamilisha ushindi wa Super Eagles.
Super Eagles itakutana na DR Congo katika mechi ya fainali ya mchujo ya Kombe la Dunia, itakayochezwa Novemba 16, katika Uwanja wa Prince Moulay El Hassan mjini Rabat, Morocco.
DR Congo imefuzu kucheza mechi hiyo, baada ya kuifunga Cameroon, kupitia bao la Chancel Mbemba alilofunga dakika za nyongeza.