Prime
Kete ya mwisho! Dakika 90 zitaamua Mbweni, KMC Complex
KWA miezi tisa, mashabiki wa soka Tanzania wamekuwa wakishuhudia ushindani wa hali ya juu Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026.
Kila raundi imekuwa na simulizi yake, kila uwanja umeandika historia yake, huku timu zikibadilishana nafasi kwenye msimamo na wachezaji wakipambana kuandika majina yao kwenye vitabu vya kumbukumbu, lakini sasa kile kilichoanza kinafikia mwisho wake.
Jumanne hii ya Juni 30, 2026, pazia la ligi hiyo linafungwa kwa mechi zote nane kupigwa kwa wakati mmoja, tofauti na raundi nyingine zilizopita, safari hii hakuna nafasi ya kusubiri kesho wala keshokutwa kurekebisha makosa, kila kitu kitaamuliwa ndani ya dakika 90.
Ni dakika ambazo zinaweza kubadilisha historia, maisha ya makocha, thamani ya wachezaji na furaha au majonzi ya maelfu ya mashabiki, dakika ambazo zinaweza kuifanya timu isherehekee ubingwa au ianze safari ya Championship, pia ni dakika ambazo zinaweza kumfanya mchezaji amalize msimu akiwa shujaa au apoteze tuzo aliyokuwa akiisaka kwa miezi kadhaa.
Licha ya baadhi ya nafasi kufahamika tayari, bado kuna vita nne kubwa hazijapata mshindi, vita hizo ndizo zitakazoifanya raundi ya mwisho kuwa moja ya raundi zenye presha kubwa zaidi.
YANGA AU SIMBA?
Hakuna vita inayovuta hisia kubwa kuliko mbio za ubingwa kati ya watani wa jadi Yanga na Simba.
Baada ya kucheza mechi 29 kila moja, Yanga ndiyo inayoongoza msimamo ikiwa na pointi 72 huku Simba ikifuatia ikiwa na pointi 70, tofauti hiyo ya pointi mbili inaifanya Yanga kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi lakini bado haijamaliza kazi.
Yanga itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya JKT Tanzania katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar, huo si mchezo wa kawaida kwa mabingwa hao watetezi kwa sababu wanakutana na timu ambayo imeonyesha ushindani mkubwa msimu huu licha ya kwamba haina cha kupoteza katika mchezo huo.
Kwa upande mwingine, Simba itakuwa mwenyeji wa KMC katika Uwanja wa KMC Complex, Dar, KMC tayari imepoteza nafasi ya kubaki Ligi Kuu Bara lakini hilo halimaanishi itakuwa mechi rahisi kwa Wekundu wa Msimbazi ambao wanajua hawana nafasi ya kufanya makosa.
Hesabu za ubingwa ziko wazi, Yanga ikishinda hakuna kitakachozuia kutwaa ubingwa wa tano mfululizo, sare pia inaweza kuitosha kutokana na tofauti ya pointi ilizonazo, ilimradi isimpe Simba nafasi ya kuipiku kwa hesabu za mwisho, Simba yenyewe haina chaguo zaidi ya kushinda kwanza, kisha kusubiri matokeo kutoka Mbweni.
Hiyo ndiyo sababu macho ya mashabiki wengi yatakuwa yakihama kutoka KMC Complex hadi Mbweni wakisubiri taarifa za kila bao litakalofungwa.
VITA YA KUSALIA
Ikiwa juu kuna hesabu za kutafuta ubingwa, chini ya msimamo kuna vita ya uhai, KMC tayari imeshuka daraja baada ya kushindwa kukusanya pointi za kutosha, lakini nafasi nyingine ya kushuka moja kwa moja bado ipo wazi.
Mtibwa Sugar ndiyo ipo kwenye wakati mgumu zaidi ikiwa na pointi 27, ili kubaki na matumaini, italazimika kupata ushindi dhidi ya Namungo huku ikisubiri matokeo ya wapinzani wake.
Tanzania Prisons yenye pointi 29, nayo haijatulia, safari yake ya Kigoma kuvaana na Mashujaa ni moja ya mechi zenye presha kubwa kwani matokeo mabaya yanaweza kuipeleka moja kwa moja Championship au kwenye mchujo.
Mbeya City nayo ipo kwenye hali kama hiyo, ikiwa na pointi 29, itahitaji kufanya vizuri nyumbani dhidi ya TRA United ili kuhakikisha haiingii kwenye hesabu mbaya za mwisho.
Tofauti ya pointi kati ya timu hizi ni ndogo kiasi kwamba bao moja linaweza kubadili msimamo wa ligi kwa dakika chache ndiyo maana kila kocha atakuwa akifuatilia si mchezo wake pekee bali pia matokeo yanayotoka viwanja vingine.
ENEO LA MCHUJO
Ingawa Namungo na Fountain Gate zipo nje ya mstari wa kushuka daraja, bado hazijajihakikishia usalama wa asilimia zote.
Namungo ina pointi 31 katika nafasi ya 11, itakuwa nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar iliyopo nafasi ya 15, ushindi utaiondoa Namungo kabisa kwenye presha lakini matokeo mabaya yanaweza kuifanya iingie kwenye mchujo endapo timu zilizo chini yake zitashinda. Hata sare, ni nafuu kwao.
Fountain Gate yenye pointi 30 nafasi ya 12, nayo haipo salama, itakuwa na mechi dhidi ya Singida Black Stars ambayo bado ina kikosi chenye uwezo mkubwa wa kuadhibu makosa madogo.
Timu hizi haziingii uwanjani kwa ajili ya kutimiza ratiba, zinacheza kuhakikisha hazimalizi msimu kwenye nafasi ya 13 au 14 ambazo zinamaanisha kucheza mechi za mchujo ili kujinusuru kushuka daraja.
FEI TOTO, OKELLO AU MOSSI?
Mbali na ushindani wa timu, kuna pambano lingine linalowakutanisha nyota watatu waliotoa burudani kubwa msimu huu.
Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ anaongoza orodha ya wafungaji akiwa na mabao 15.
Nyuma yake kuna Allan Okello wa Yanga ambaye amepanda kwa kasi baada ya kufunga hat-trick dhidi ya TRA United na kufikisha mabao 14.
Idadi hiyo pia anayo Mossi Nduwumwe wa Singida Black Stars ambaye kabla ya kusimamishwa na Simba katika mechi iliyopita ya ligi alifunga mabao matano katika mechi mbili za ligi.
Fei Toto atakuwa akiongoza safu ya ushambuliaji ya Azam dhidi ya Dodoma Jiji huku akisaka kuongeza idadi ya mabao yake.
Okello naye atakuwa na kazi mbili kwa wakati mmoja kuiongoza Yanga kutetea ubingwa na wakati huohuo kuisaka tuzo ya mfungaji bora.
Kwa Mossi, mchezo dhidi ya Fountain Gate unaweza kuwa nafasi yake ya kuwazidi kete Feisal na Okello.
MECHI ZISIZO NA PRESHA
Kuna mechi zingine zinapigwa leo hazina presha zaidi ya timu kupambania kumaliza eneo zuri kwenye msimamo kwani kuna fedha zinatolewa kwa kiwango tofauti na wadhamini wa ligi hiyo.
Kuanzia nafasi ya kwanza hadi ya mwisho, mdhamini mkuu wa ligi hiyo na yule wa upande wa haki za matangazo, wanatoa fedha viwango tofauti kwa timu kulingana na nafasi.
Anachopokea bingwa, sio sawa na kile anachopata anayeshika nafasi ya pili wala ya tatu. Lakini zile mbili zinazoshuka daraja moja kwa moja kwa maana ya nafasi ya 15 na 16, kiwango chao ni sawa.
Kumbuka zawadi hizo zilitangazwa tangu msimu wa 2021-2022 ambapo bingwa jumla anaondoka na Sh600 milioni, nafasi ya pili (Sh300 milioni), nafasi ya tatu (Sh255 milioni), nafasi nne (Sh200 milioni), nafasi ya tano (Sh65 milioni), nafasi ya sita (Sh60 milioni), nafasi ya saba (Sh55 milioni), nafasi ya nane (Sh50 milioni), nafasi ya tisa (Sh45 milioni), nafasi ya kumi (Sh40 milioni), nafasi ya 11 (Sh35 milioni), nafasi ya 12 (Sh30 milioni), nafasi ya 13 (Sh25 milioni), nafasi ya 14 (Sh20 milioni) nafasi ya 15 (Sh10 milioni), nafasi ya 16 (Sh10 milioni). Timu yenye nidhamu Sh20 milioni.
Coastal Union itakayoikaribisha Pamba Jiji kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, hakuna ambayo ipo kwenye presha ya kushuka. Coastal inashika nafasi ya tisa na pointi 33 ambazo haziwezi kufikiwa na timu iliyo kwenye hatari ya kushuka moja kwa moja, wala zile za mtoano. Inachopambana ni kushinda ili kupanda nafasi ya juu na endapo itafunga mabao mengi, maana yake itaishusha Pamba Jiji kwa tofauti ya mabao. Hivi sasa Pamba Jiji ina pointi 36 ikiwa nafasi ya saba, tofauti yao ni pointi tatu na mabao matano.
Azam iliyojimilikisha nafasi ya tatu ikikusanya pointi 61, itaikaribisha Dodoma Jiji iliyopo nafasi ya nane na pointi 35.
Kupoteza kwa Dodoma Jiji mechi hii, kuna hatari ya kushuka nafasi moja, endapo Coastal na Mashujaa zikishinda, lakini timu hiyo haitashuka daraja kwani ipo salama hadi sasa. Mechi hii itachezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar.
WASIKIE WADAU
Nahodha wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi amesema kwa ujumla ligi imekuwa na changamoto nzuri ya ushindani, lakini kuhusu nani anamuona anastahili kuchukua MVP msimu huu inakuwa ngumu kwa nafasi yake kufanya uchaguzi huo.
“Mimi ni tofauti na mchambuzi, naweza nikataja mchezaji ninayemuona anastahili halafu asipate, watu wanaanza kutolea mfano kwamba hata Mgosi aliwahi kusema na kuona wahusika wanapendelea,” amesema Mgosi na kuongeza.
“Nawapongeza Bodi ya Ligi Tanzania na TFF zimefanya ligi iwe bora na yenye mvuto, ndiyo maana kila mtu anasubiri nani atakuwa bingwa pia timu zimezidiana pointi chache hata zile zilizopo chini kwenye msimamo wa ligi, hivyo mojawapo ikidondosha pointi mechi za mwisho itakuwa imekula kwake.
“Ninachoshauri watu wafanye promo kwa wachezaji wanaostahili na siyo kwa sababu mtu anashabikia timu fulani ama yupo karibu na fulani, kwa ajili ya maendeleo ya mpira lazima kila mtu apate anachostahili.”
Kwa upande wa beki wa zamani wa Yanga, Oscar Joshua, amesema: “Ligi imebakia na mvuto mkubwa hadi mechi ya mwisho ndipo itajulikana kati ya Yanga na Simba nani bingwa, pia itajulikana timu gani zinashuka au kucheza mtoano ukiondoa KMC ambayo ilishashuka, kuhusu nani mchezaji bora zipo kamati zinazoshugulikia hilo.”
Staa mwingine wa zamani wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma, amesema: “Kwa upande wangu mchezaji ninayemuona amekuwa na muendelezo wa kiwango ni kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye ndiye kinara wa mabao 15, asisti nane, ila kwa ujumla ligi ni nzuri na bora.”
Mtazamo wa staa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Steven Mapunda, amesema: “Anayestihili kuwa MVP vinaangaliwa vitu vingi, ikiwemo pafomansi yake, hilo lipo chini ya watu wa kamani ya tuzo, ila ligi kwa ujumla ina mvuto, imetubidi kusubiri hadi mwisho kujua nani bingwa, timu ipi inaifuata KMC kushuka na zipi zitacheza mtoano.”
KAULI ZA MAKOCHA, WACHEZAJI
Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amesema maandalizi yanaendelea vizuri licha ya safari ndefu kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam, akieleza kuwa kipaumbele kikubwa ni kuwapa wachezaji muda wa kupumzika na kurejesha nguvu kabla ya mchezo.
Amesema wachezaji wote wako katika hali nzuri kiafya isipokuwa Edson Katanga ambaye atakosekana kutokana na adhabu ya kadi.
“Mchezo utakuwa mgumu kwa sababu kila timu ina malengo yake. Sisi tupo hapa kwa ajili ya kutimiza malengo ya JKT, si kuangalia timu nyingine zinafanya nini. Tutacheza kwa nidhamu ya kimkakati na kuhakikisha tunafanya kila tuwezalo kupata matokeo mazuri,” amesema Ally.
Kwa upande wa nyota wa JKT, Nassor Maulid, amesema morali ndani ya kikosi ipo juu na wachezaji wamejipanga kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ili kufanikisha malengo ya timu.
“Sisi tuna malengo yetu kama ambavyo wapinzani wetu wana malengo yao. Tutapambana kuhakikisha tunamaliza msimu kwa matokeo mazuri,” amesema.
Wakati huo huo, Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin, amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo muhimu ambao unaweza kuipa timu ubingwa wa Ligi Kuu.
Moallin amesema wachezaji wote wako fiti na wana morali ya juu, huku akisisitiza kuwa wanafahamu ubora wa JKT kutokana na michezo ya awali iliyowakutanisha.
“JKT ni timu nzuri yenye kocha bora na iliyopangwa vizuri. Tunafahamu uwezo wao, hivyo tunapaswa kucheza kwa kiwango cha juu na kuwa makini hasa upande wa ulinzi. Lengo letu ni kushinda mchezo na kusherehekea ubingwa baada ya hapo,” amesema.
Naye mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Mwanengo, amesema mchezo huo ndio unaoamua hatima ya ubingwa wa timu yao.
“Hata ushindi wa bao moja unatosha kutupa ubingwa. Tunaamini mbele ya mashabiki wetu tutafanya vizuri na kumaliza kazi,” amesema.
Beki wa Simba, Shomari Kapombe, amesema ushindani wa msimu huu umekuwa mkubwa na timu imepitia changamoto nyingi, lakini imefanikiwa kuzivuka.
“Lengo letu ni kupata pointi tatu katika mchezo wa mwisho na kuwafurahisha mashabiki wetu ambao wamekuwa nasi tangu mwanzo wa msimu. Tunawaomba wajitokeze kwa wingi kwa sababu wao ni mchezaji wetu wa 12,” amesema Kapombe.
Kapombe pia amepongeza usajili uliofanyika dirisha dogo akisema wachezaji wapya wameongeza nguvu kubwa ndani ya kikosi na kutoa mchango muhimu katika mafanikio ya timu.
Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, amesema licha ya KMC kushuka daraja, mchezo dhidi yao hautakuwa mwepesi kwani kila mchezaji wa wapinzani atataka kujitangaza kwa ajili ya kupata timu msimu ujao.
“Kushuka daraja ni kwa timu, si kwa wachezaji. Kila mmoja atapambana kuonyesha uwezo wake, hivyo tunatarajia mchezo mgumu lakini sisi tunahitaji pointi tatu,” amesema Matola.
Kwa upande wa KMC, kocha wa timu hiyo, Iman Mwalupetelo amesema wachezaji wa kikosi hicho bado wana sababu ya kupambana licha ya kushuka daraja, huku mchezaji Jammy Simba akieleza kuwa timu imepitia kipindi kigumu na sasa italazimika kujipanga upya kwa ajili ya kurejea ikiwa na nguvu zaidi msimu ujao.
NENO LA WADHAMINI
Wadhamini wakuu wa Ligi Kuu, Benki ya NBC, wametangaza kuwa wameandaa sherehe mbili za ubingwa zenye viwango sawa ili kuhakikisha bingwa atakayepatikana anakabidhiwa kombe haraka.
NBC ilieleza kuwa, helikopta itatumika kusafirisha kombe kwenda kwenye uwanja ambao bingwa atapatikana, hatua inayolenga kuifanya ligi iendeshwe kwa viwango vya kimataifa na kuhakikisha sherehe za ubingwa zinafanyika siku hiyo hiyo bila kuchelewa.
Akizungumzia hilo, Mkuu wa Idara ya Masoko wa NBC, David Raymond, amesema: “Maswali yamekuwa mengi sana kwamba tutafanyaje ili kuweza kukamilisha. Kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi na TFF sisi kama wadhamini tukasema kwa ubora wa ligi yetu tuna wajibu wa kuhakikisha ya kwamba tunakwenda kuandaa sherehe mbili ambazo ziko na viwango sawa kabisa kwa maana ya kwamba popote ambapo mshindi atapatikana basi ataweza kukabidhiwa kombe lake pale pale uwanjani.
“Hivyo basi, katika namna ya kuboresha na kuhakikisha hili linatokea, tutakuwa na helikopta ambayo itaweza kubeba hili kombe na kulifikisha kwa wakati kwenye uwanja husika ambapo mshindi atakuwa amepatikana. “Hii yote ni kuendana na viwango vya kimataifa kama ambavyo tumesema lakini kuhakikisha kwamba mshindi anapata kombe lake siku hiyo hiyo. Ligi yetu imekuwa kubwa sana, kwa hiyo lazima twende na viwango na sisi kama wadhamini kwa sababu ya ukubwa wa chapa yetu na ukubwa wa benki yetu nchini tukasema basi hili ni jambo ambalo inabidi kuliendea na kuhakikisha kuwe na viwango vinavyostahili.
“Kwa mashabiki na wakazi wa jiji la Dar es Salaam wataona chopa ikiwa angani ikisubiri maelekezo ya waendesha soka wakituambia kwamba ni wapi itue na wapi iweze kupeleka kombe ili mshindi akabidhiwe.”