Thibaut Courtois ataja walinda mlango watatu bora duniani
Muktasari:
- Courtois ambaye amewahi kuzitumikia Chelsea na Atletico Madrid, ametaja orodha hiyo ya makipa watatu, akiwa katika mahojiano maalum kwenye kituo cha redio cha COPE nchini Hispania.
Kipa wa timu ya taifa ya Ubelgiji na klabu ya Real Madrid, Thibaut Courtois, ametaja orodha ya makipa bora, ambao anaamini kwa sasa wanafanya vizuri katika soka la ushindani.
Courtois ambaye amewahi kuzitumikia Chelsea na Atletico Madrid, ametaja orodha hiyo ya makipa watatu, akiwa katika mahojiano maalum kwenye kituo cha redio cha COPE nchini Hispania.
Hata hivyo, kwenye orodha hiyo, Courtois amejiondoa kwa kuamini yeye bado ni bora, lakini aliowataja anaamini wana kiwango cha kumpa ushindani katika soka la sasa, ambalo limekuwa na mvuto zaidi.
Kipa huyo mwenye umri wa miaka 33, amemtaja Jan Oblak wa Atletico Madrid, David Raya wa Arsenal na Alisson Becker wa Liverpool.
Amesema: “Kwa sasa, Jan Oblak anacheza kwa kiwango cha juu sana mwaka huu. Ninampenda sana Alisson, ingawa yupo kwenye majeraha kwa sasa. Pia ninampenda sana David Raya.”
Ingawa Courtois anajihesabu kuwa miongoni mwa makipa bora kwa sasa, amesisitiza kuendelea kuisaidia Real Madrid kushinda mechi za mashindano yote wanayoshiriki, na mwisho wa msimu huu kutwaa mataji.
“Bila shaka mimi ni mmoja wa makipa bora kwa sasa, lakini yote yanategemea mashabiki wako wanavyokuchukulia, na kila mtu ana uhuru wa kuwa na maoni yake.
“Jukumu langu kubwa ni kuisaidia Real Madrid ili iweze kufanya vizuri katika mechi zinazotukabili msimu huu, ili tufanikishe mpango wa kutwaa mataji na kuendelea kuwa klabu bora duniani,” Courtois ameongeza.
Courtois alijiunga na Real Madrid Agosti 2018, akitokea Chelsea kwa ada ya Pauni 35 milioni. Usajili wake ulilenga kuimarisha nafasi ya mlinda mlango wa kwanza katika klabu ya Hispania, na kuendeleza historia ya Real Madrid ya kuwa na wachezaji bora duniani katika nafasi hiyo.
Tangu kujiunga kwake na klabu hiyo, Courtois amekuwa tegemeo kubwa kwenye kikosi cha kwanza, akicheza mechi 282 katika mashindano yote. Uwezo wake wa kuokoa michomo muhimu na kuongoza mstari wa nyuma umemfanya kuwa mmoja wa makipa bora duniani na tegemeo kwa Real Madrid.
Katika kipindi hiki, amechangia kwa kiwango kikubwa kwenye mafanikio ya klabu, ikiwa ni pamoja na kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya, La Liga.