Karim Benzema: Nipo tayari kurudi Real Madrid
Muktasari:
- Benzema aliondoka kwa mabingwa hao wa LaLiga kama mchezaji huru Julai 2023 na kujiunga na Saudi Pro League ambayo ni ligi maarufu ya Mashariki ya Kati.
Mshambuliaji wa Ufaransa na klabu ya Al Ittihad ya Saudi Arabia, Karim Benzema, amesema yupo tayari kurudi Real Madrid, endapo itatokea nafasi hiyo.
Benzema aliondoka kwa mabingwa hao wa LaLiga kama mchezaji huru Julai 2023 na kujiunga na Saudi Pro League ambayo ni ligi maarufu ya Mashariki ya Kati.
Katika mahojiano na gazeti la AS, Benzema amekiri itakuwa vigumu kwake kukataa kurejea Real Madrid, endapo rais wa klabu hiyo, Florentino Pérez, atamuomba afanye hivyo.
“Kama Florentino [Pérez] bado yuko pale, inaweza kutokea, inaweza kutokea kabisa, na mimi sitakuwa na kipingamizi chochote. Ninamzungumzia na inawezekana.
"Mimi ni shabiki wa Real Madrid. Ninahisi hivyo moyoni mwangu. Real Madrid bado ni jiji langu, najihisi kama shabiki wa Real Madrid na kama Mmadrid,” amesema Benzema.
Ameongeza kuwa, atasubiri kuona kitakachotokea, akimaanisha hilo linaweza kutegemea uwepo wa Rais Pérez.
Benzema alijiunga na Real Madrid mwaka 2009 akitokea Olympic Lyon ya Ufaransa, akisajiliwa kwa ada ya Euro 35 milioni.
Alitua Real Madrid akiwa na umri wa miaka 21 na alianza kuonyesha ubora wake kama mshambuliaji wa kimataifa. Katika kipindi chake cha miaka 14 ndani ya Los Blancos, alishinda mataji mengi ya LaLiga, Ligi ya Mabingwa Ulaya, na tuzo binafsi ikiwemo Ballon d’Or, akijenga jina lake kama mmoja wa washambuliaji bora wa karne hii.
Akiwa na Real Madrid kuanzia 2009 hadi 2023, Karim Benzema alicheza mechi 648 na kufunga mabao 354. Hii inamweka Benzema miongoni mwa washambuliaji wakubwa zaidi katika historia ya klabu hiyo.
Baada ya kuhamia Al Ittihad, Benzema amecheza mechi 58 za mashindano yote, huku akitoa michango wa mabao 50, akifunga 33 na kuasisti 17. Mkataba wake na Al Ittihad unamalizika Juni 2026.