Ten Hag kaanzia alipoishia huko
Muktasari:
- Kocha huyo Mdachi alifutwa kazi na Manchester United, Oktoba mwaka jana baada ya kushinda mechi tatu tu kati ya tisa za kwanza kwenye Ligi Kuu England, huku kipigo kutoka kwa West Ham ndicho kilichohitimisha zama zake Old Trafford.
RIO DE JANEIRO, BRAZIL: KOCHA, Erik ten Hag ameendelea alipoishia baada ya kukumbana na kichapo kwenye mechi yake ya kwanza kuinoa Bayer Leverkusen huku mbaya zaidi akipoteza mbele ya timu ya vijana.
Kocha huyo Mdachi alifutwa kazi na Manchester United, Oktoba mwaka jana baada ya kushinda mechi tatu tu kati ya tisa za kwanza kwenye Ligi Kuu England, huku kipigo kutoka kwa West Ham ndicho kilichohitimisha zama zake Old Trafford.
Na tangu hapo Ten Hag alikuwa hana timu hadi ilipofika Mei mwaka huu alipotangazwa kurithi mikoba ya Xabi Alonso huko Leverkusen.
Lakini, mechi yake ya kwanza baada ya kurudi kwenye benchi la ufundi iliisha kwa majanga makubwa licha ya Leverkusen kupewa nafasi kubwa ya kushinda mechi hiyo kabla haijaanza. Leverkusen ilisafiri hadi Brazil kwenda kumenyana na Flamengo, ambayo ni mechi ya kwanza ya Ten Hag baada ya kupata kazi mpya.
Hata hivyo, Flamengo yenyewe ilikuwa ni ya kikosi cha U20 sio kile cha wakubwa. Lakini, wakali hao wa Brazil hawakushindwa kuisambaratisha Leverkusen kwa kipigo cha mabao 5-1.
Ten Hag alianza na kikosi chake cha mastaa wa maana kabisa akiwamo Mark Flekken, Jonas Hoffman na Victor Boniface na kutumia mfumo uleule wa mtangulizi wake Alonso wa 3-4-2-1. Lakini, ndani ya sekunde tu, Flamengo ikafunga bao la kuongoza kabla ya kuongeza la pili kwenye dakika 10, kitu kilichomfanya kocha Ten Hag kuamua kufanya mabadiliko ya kuwatoa Flekken na Boniface kwenye dakika ya 36 tu ya mchezo.
Flamengo ilizidi kukanyagia, ikafunga bao la tatu kabla ya kuongeza la nne ubao kusomeka 4-0 sekunde chache kabla ya filimbi ya mapumziko. Ten Hag hakufanya mabadiliko mengine wakati wa mapumziko na dakika 10 baadaye, baada ya mechi kuanza kwenye kipindi cha pili, Flamengo ilifunga bao la tano. Kwenye dakika 60, Ten Hag alitoa wachezaji wote uwanjani, wakiwamo wale wawili waliokuwa wameingia, hivyo akawaingiza Granit Xhaka, Alex Grimaldo na Patrick Schick kabla ya Montrell Culbreath kufunga bao la kujifariji katika dakika ya 71.