Ten Hag azuia pesa, Neymar huyoo

MANCHESTER, ENGLAND. KOCHA wa Manchester United, Erik ten Hag amewaonya mabosi wa timu hiyo kutotumia pesa kwa fujo kama ilivyokuwa kwa Chelsea ikiwa timu itauzwa.
Ten Hag ametoa kauli hiyo baada ya kuahidiwa kwamba atapewa pesa nyingi ya kufanyia usajili ikiwa timu hiyo itauzwa kwa Sir Jim Ratcliffe au Sheikh Jassim Bin Hamad Al Thani mwaka huu.

Hata hivyo, kocha huyu bado anatamani kuona staa wa kimataifa wa Brazil, Neymar akisajiliwa kwenye kikosi hicho ingawa hataki kuona pesa nyingi zikitumika kwenye hilo.
Chelsea imetumia zaidi ya Pauni 600 milioni kwenye kufanya usajili wa wachezaji wapya mara baada ya timu kuuzwa kwa Todd Boehly aliyeinunua kwa Pauni 4.25 bilioni kutoka kwa Roman Abramovich.

Ten Hag amesema kwamba wanatakiwa wawe na akili kubwa kwenye kufanya usajili na kusuka upya kikosi bila ya hivyo wanaweza kujikuta kwenye wakati mbaya kwani kuwa na pesa peke yake haitoshi.
"Kwa sasa unaweza kusema kweli kuna wachezaji bora, makocha bora na pesa nyingi sana hapa Uingereza hali inayosababisha kuwe na ushindani wa kutosha, lakini unatakiwa ufanye vitu kwa usahihi na hata kama ukitumia pesa utumie kwa njia nzuri na mipango imara, bila ya hivyo pesa yako haitakupa matokeo yoyote."

Erik pia alikataa kukanusha tetesi zinazoihusisha timu hiyo na usajili wa staa wa kimataifa wa Brazil, Neymar ambaye taarifa zinadai mabosi wa Paris Saint-Germain wamepanga kumuuza katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Neymar ambaye alijiunga na PSG kwa Pauni 200 milioni mwaka 2017 akitokea Barcelona, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2025 lakini PSG inataka kumuondoa kwenye timu na kuanza kujenga upya kikosi chao kwa wachezaji vijana.
"Pale kutakapokuwa na taarifa yoyote tutawaambia," alisema Ten Hag kujibu moja ya swali la mwandishi kuhusiana na ishu hii ya Neymar.

Neymar ambaye pia anahusishwa na kurejea Barcelona, tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 20 za Ligi Kuu ya Ufaransa na amehusika katika mabao 24, akifunga 13 na kutoa asisti 11.
Man United inatarajiwa kuondoa kundi kubwa la wachezaji wake wa kikosi cha kwanza ikiwemo Harry Maguire, Anthony Martial, Diogo Dalot, Aaron Wan-Bissaka, Donny van de Beek, Anthony Elanga, Brandon Williams, Phil Jones, Axel Tuanzebe, Eric Bailly na Alex Telles, huku kipa wao, David de Gea hatma yake haijulikani kama atabaki ama ataondoka.

Ten Hag anadai hadi sasa hakuna mchezaji ambaye timu imefikia makubaliano ya kumuacha zaidi ya wale waliotangazwa kama Phil Jones, hivyo wanataka wamalize msimu kwanza kabla ya kufanya uamuzi wa nani na nani watabaki ama kuondoka kwenye timu.

Man United ambayo msimu huu imeshachukua taji la Carabao Cup itakuwa na kazi ngumu ya kuhakikisha inalinda rekodi yake mbele ya majirani zao Manchester City kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la FA.

Man City kwa sasa inaikimbizia rekodi ya kushinda mataji matatu makubwa ndani ya msimu mmoja ambapo kwa upande wa England iliwahi kuwekwa na Man United pekee mwaka 1999.
Man City ambayo imeshachukua taji la Ligi Kuu England, ipo kwenye fainali nyingine mbili ikiwa ile ya FA na Ligi ya Mabingwa ambapo kama ikishinda basi itakuwa imefikia kilichowahi kufanywa na Man United.