Tajiri akianza kazi Man United nani atabaki, ataondoka Old Trafford

Muktasari:

  • Na sasa kitu kinachowahusu ni ujio wa bilionea mpya, tajiri Sir Jim Ratcliffe na hatima ya mastaa wa timu hiyo katika mipango yake ya uwekezaji. Kipi kitatokea baada ya bilionea huyo kutua Old Trafford?

MANCHESTER ENGLAND: Manchester United siku zote inakuwa na kitu cha kuzungumzwa. Kinaweza kuwa kizuri kwao au cha kubezwa. Lazima wawe na kitu.

Na sasa kitu kinachowahusu ni ujio wa bilionea mpya, tajiri Sir Jim Ratcliffe na hatima ya mastaa wa timu hiyo katika mipango yake ya uwekezaji. Kipi kitatokea baada ya bilionea huyo kutua Old Trafford?
Gwiji wa miamba hiyo mabingwa mara 20 wa ligi, Gary Neville anaamini mabadiliko makubwa yanakuja kutokea kwenye timu hiyo, hasa yakilenga mambo ya uwanjani, hivyo amewaonya mastaa wa kikosi hicho baada ya ushindi usioridhisha wa mabao 2-1 dhidi ya Luton, wasipojiangalia, itakula kwao.

Neville alisema: “Ujio wa Ratcliffe ni kama anawaambia wachezaji ‘namtazama kila mmoja, hivyo mnacheza kwa ajili ya hatima zenu’.”

Mabadiliko makubwa yanatarajia kutokea Old Trafford ikiwamo ujio wa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu mpya pamoja na Mkurugenzi wa soka na kwa sasa utakuwa chini ya kampuni ya tajiri huyo, Ineos, lakini kila mchezaji anavyocheza kwa sasa ni kama mbegu aliyopanda na mavuno yake yatapatikana dirisha lijali la usajili.
Tunakipitia kikosi cha Man United na kuchambua kila mchezaji kuona kile ambacho anafanya kwenye timu hiyo kwa sasa kinastahili kuendelea kubaki kwenye kikosi hicho kwa ajili ya matumizi ya baadaye au ni wakati wa kufunguliwa mlango wa kutokea na kupisha mastaa wapya.

Andre Onana, kipa
Amebadilika sana na siku za karibuni ameonyesha ni mchezaji anayestahili kuendelea kuwapo kwenye goli la miamba hiyo. Mwanzoni mwa msimu wasiwasi ulikuwa mkubwa kama ni chaguo sahihi kwenye kikosi hicho, lakini kiwango cha hivi karibuni kimeonyesha Dhahiri subira inavuta heri. ABAKI.

Altay Bayindir, kipa
Alipewa nafasi moja ya kuonyesha kile anachoweza kuipa Man United anapokuwa na jezi ya timu hiyo, hivyo ni ngumu kumhukumu kama anafaa au hafai. Hivi karibuni kuliibuka ripoti anaweza kutolewa kwa mkopo mwisho wa msimu, lakini kama hakuna ulazima hana shida ya kuwepo. APEWE MUDA

Tom Heaton, kipa
Kipa veterani, ni chaguo cha pili zuri la kipa kwenye kikosi cha Man United hasa ukizingatia hata mshahara wake si mkubwa. Umri wake ni miaka 37 na mwenyewe hana shida kwa kuwa chaguo la pili, huku uwepo wake kwenye timu ukiongeza uzoefu kwenye kikosi kuwafunza makipa wanaochipukia. ABAKI.

Aaron Wan-Bissaka, beki wa kulia
Ameshindwa kuifanya nafasi ya beki wa kulia ni ya kudumu kwake kwa sababu moja au nyingine. Kwenye kikosi cha Man United mkataba wake utafika tamati majira ya kiangazi 2025 na uwepo wa Diogo Dalot unakuwa kikwazo kwa beki huyo wa zamani wa Crystal Palace. Kwa hali ilivyo, hana chake. ATOKE.

Diogo Dalot, beki wa kulia
Amekuwa mchezaji anayetumika sana kwenye kikosi cha Man United chini ya Kocha Erik ten Hag. Wakati mwingine amekuwa akipangwa kwenye beki ya kushoto, huku beki ya kulia akiwa amejihakikishia nafasi. Kwenye maandalizi ya kuunda safu mpya ya mabeki ya Man United, ni mwanzo wa yote. ABAKI.

Raphael Varane, beki wa kati
Amerejea kwenye kikosi cha kwanza cha Man United baada ya kujikuta akiwekwa benchi mwanzoni mwa msimu. Shida kubwa inayomsumbua Mfaransa huyo ni majeraha ya mara kwa mara, akishindwa kuitumikia timu ipasavyo huku mshahara wake ukiwa ni mkubwa. Waarabu wanamhitaji na bila shaka atauzwa. ATOKE.

Harry Maguire, beki wa kati
Staa mwingine aliyepambana sana kurejea kwenye kikosi cha kwanza cha Man United ni beki huyu wa kati. Siku za kati alionekana kutulia, lakini alifanya makosa kwenye mechi za Luton na West Ham yameanza kuibua hofu tena bado Man United haipo salama chini ya beki huyo. Bado haipi kitu Man United. ATOKE.

Victor Lindelof, beki wa kati
Ni mchezaji mwingine ambaye atabakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake itakapofika mwisho wa msimu huu. Ni mchezaji mwingine ambaye Man United haitakuwa kwenye hasara yoyote endapo kama itamfungulia mlango wa kutokea. Beki huyo bado ana uwezo, Man United inaweza kumuuza ili asiondoke bure. ATOKE.

Lisandro Martinez, beki wa kati
Bila shaka ni beki bora kabisa kwenye kikosi cha Man United kwa sasa na ni sehemu muhimu ya maisha ya Man United kwa siku za baadaye. Kitu ambacho Man United inapaswa kukifanya kwa Martinez ni kumlinda asipate majeraha ya mara kwa mara. Kingine ni kumtumia kwenye nafasi ambayo itamfanya aonyeshe ubora. ABAKI.

Jonny Evans, beki wa kati
Ni rahisi sana kuwepo kwenye kundi la wanaopaswa kubaki, lakini umri ni kitu ambacho kinamtupa mkono. Ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa kwenye Ligi Kuu England na hicho amekuwa akikionyesha kwenye timu hiyo msimu huu. Msimu huu Man United inatumia uzoefu wake lakini si zaidi. ATOKE.

Luke Shaw, beki wa kushoto
Anapokuwa fiti, ni mmoja wa mabeki wa kushoto bora kabisa duniani, hivyo kuendelea kubaki Old Trafford halitakuwa tatizo. Lakini, tatizo linalomkabili Shaw ni majeraha ya mara kwa mara jambo linalowafanya Man United kuanza kutafuta mbadala wake wa kudumu. Kwa kipindi hiki, hakuna namna Shaw ni muhimu kikosini. ABAKI.

Tyrell Malacia, beki wa kushoto
Kuzungumzia ushindani wake wa namba na Shaw, anapaswa kuendelea na mapambano katika kumfanya Kocha Ten Hag aendelee kumpa nafasi. Majeraha yamemtibulia sana maisha yake, lakini umri wake bado unampa nafasi ya kuendelea kuichezea timu hiyo ya Old Trafford kwa muda mrefu. APEWE MUDA.

Casemiro, kiungo wa kati
Msimu uliopita alikuwa kwenye kiwango bora sana, lakini msimu huu amekuwa mchezaji wa kawaida, akifanya makosa mengi ndani ya uwanja na hivyo, huku akionyeshwa kadi ambazo zinaigharimu timu. Man United kwa sasa ina huduma ya kiungo matata kabisa, Kobbie Mainoo na wengine inaowasaka hivyo Casemiro si shida. ATOKE. 

Christian Eriksen, kiungo wa kati
Alisajiliwa kwa uhamisho wa bure kabisa na lilikuwa ni ingizo muhimu kwenye kikosi. Hivi karibuni alihusishwa na mpango wa kutaka kuachana na timu hiyo na ilidaiwa angekwenda Uturuki. Ukweli ni kiwango chake kwa sasa si kama zamani na si mchezaji wa kumtumia kwa dakika zote tisini kwenye mechi. ATOKE.

Kobbie Mainoo, kiungo wa kati
Zao la kutoka kwenye Carrington. Amekuwa gumzo kubwa kwa sasa na England wanapiga hesabu za kumjumuisha kwenye kikosi chao cha timu ya taifa kutokana na soka analopiga. Kwa sasa kiungo ya Man United imekuwa kwenye mikono salama kutokana na uwepo wa kinda huyo, ambaye bila shaka atapewa muda. ABAKI.

Bruno Fernandes, kiungo mshambuliaji
Amekuwa mchezaji bora wa Man United tangu alipojiunga na timu hiyo miaka minne iliyopita. Ameendelea kuwa mchezaji bora linapokuja suala la kutengeneza nafasi za mashambulizi ndani ya uwanja. Ndiye nahodha wa timu hiyo na ubora wake bado unampa nafasi ya kuendelea kucheza kwenye kikosi hicho cha Old Trafford. ABAKI.

Mason Mount, kiungo mshambuliaji
Alianza vyema maisha yake mapya huko Man United kabla ya kutibuliwa na majeruhi yaliyomfanya awe nje ya uwanja kwa muda mrefu. Ubora wake uliongeza kitu kwenye kiungo ya Man United na kocha Ten Hag alionekana kumwamini zaidi huku akiwa na mkataba kwenye timu hiyo hadi 2025. APEWE MUDA.

Scott McTominay, kiungo wa kati
Kama kuna wachezaji waliokuwa wakipigiwa hesabu za kuuzwa kwenye kikosi cha Man United basi ni huyu. Lakini, kwa sasa mkali huyo anatumika kama silaha inayobaki kwenye benchi la kocha Ten Hag na anapoingia muda wowote anabadili matokeo. Kwa kila anachokifanya bado anahitajika. ABAKI.

Sofyan Amrabat, kiungo wa kati
Alibeba matarajio makubwa sana wakati anatua Man United akitokea Fiorentina hasa baada ya kiwango chake matata kabisa alichokionyesha kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar alipokuwa na Morocco. lakini, staa huyo bado hajaonyesha kitu kikubwa Old Trafford anakocheza kwa mkopo, hawezi kubaki. ATOKE.

Marcus Rashford, mshambuliaji
Miongoni mwa mastaa wa Man United ambao ubora wao ni mkubwa na unaweza kuwategemea kwa kuwa na huduma nzuri uwanjani. Hivi karibuni alikuwa na matatizo ya nje ya uwanja ambayo yamemfanya ashindwe kuonyesha kiwango kizuri kwenye mechi, lakini si mchezaji wa kumkosa kikosini. ABAKI.

Alejandro Garnacho, mshambuliaji
Ni mshambuliaji ambaye ameifanya winga ya kushoto au kulia kuwa eneo lake la kuonyesha kiwango bora kabisa tangu alipoanza kuitumikia Man United. Bado kijana mdogo na amekuwa akitengeneza ushirikiano mzuri na wakali wengine kama Rashford na Rasmus Hojlund kwenye fowadi ya timu. ABAKI.

Rasmus Hojlund, mshambuliaji
Baada ya kuanza kwa kasi hafifu, kwa sasa amewasha moto kwenye kikosi cha Man United akifunga mabao kwa kadri anavyotaka. Kitu ambacho anahitaji ni pacha wake tu kwenye fowadi ambaye watagawana majukumu kwenye kufunga mabao ili kuisaidia timu yao kufanya vizuri. Ni kijana na mahiri. ABAKI.

Antony, mshambuliaji
Dau kubwa lililotumika kunasa saini yake linaonekana kumtesa winga huyu wa Kibrazili. Mchezaji huyo angeweza kusajiliwa kwa Pauni 25 kutokana na thamani yake sokoni, lakini Man United ilipigwa pesa nyingi sana na Ajax na hakuna kitu ambacho anafanya cha maana kwenye kikosi hicho cha Old Trafford. Hajielewi. ATOKE.

Anthony Martial, mshambuliaji
Mwishoni mwa msimu huu, mkataba wake utafika tamati huko Man United na kwa muda wake aliokuwa Old Trafford, staa huyo wa Ufaransa ameshindwa kabisa kufanya kitu cha maana ndani ya uwanja. Majeruhi yamekuwa yakimwandama na kumfanya akose nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Ten Hag. ATOKE.

Amad Diallo, mshambuliaji
Kama angepewa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza bila ya shaka kuna kitu angekionyesha kwenye kikosi hicho cha Man United. Winga huyo mwenye umri wa miaka 21 alitolewa kwa mkopo mara kadhaa, ambako alikwenda kuonyesha kiwango bora na kurudi Old Trafford msimu huu. Bado ana nafasi. APEWE MUDA.