Mastaa wasioimbwa NBA 2025

Muktasari:
- Wachezaji kama Tyrese Haliburton (Indiana Pacers), Aaron Gordon (Denver Nuggets), Jalen Brunson (New York Knicks) na Jimmy Butler (Miami Heat) wamekuwa wakionyesha ubora mkubwa.
TEXAS, MAREKANI: KATIKA kipindi cha mchujo (playe off) kinachoendelea kwenye Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), macho ya wengi yameelekezwa kwa nyota wanaobeba majukumu ya timu.
Wachezaji kama Tyrese Haliburton (Indiana Pacers), Aaron Gordon (Denver Nuggets), Jalen Brunson (New York Knicks) na Jimmy Butler (Miami Heat) wamekuwa wakionyesha ubora mkubwa.
Hata hivyo, mbali na mastaa hao kuna kundi la wachezaji ambao kwa kawaida hawatajwi sana, lakini wameibuka shujaa wa kweli katika safari ya mchujo.
Hao ni wale wanaoitwa “mashujaa wasioibwa sana†(unsung heroes), wachezaji waliopanda ngazi ya ubora wakati ambao timu zilihitaji msaada zaidi. Bila mchango wa wachezaji hao baadhi ya timu zisingeweza kufika hatua ya mchujo.
JARRETT ALLEN
Licha ya kuwa mchezaji wa zamani wa kikosi cha All-Star, Allen anayeichezea Cleveland Cavaliers amekuwa akitimiza majukumu kimyakimya akiwa na wastani wa alama 15 katika mchujo.
Mchango wake umekuwa mkubwa zaidi kufuatia majeraha ya Evan Mobley na kwa sasa ndiye kiongozi wa timu upande wa rebound na ulinzi. Allen ameonyesha umuhimu kuhakikisha Cavs inaendelea kupambana katika mchujo.
CHRISTIAN BRAUN
Baada ya Nuggets kutowasaini Bruce Brown na Kentavious Caldwell-Pope, Braun alipata nafasi ya kuonyesha uwezo, akiwa na dakika 39 kwa mchezo.
Jamaa anacheza kwa nguvu, anakaba na kukimbia vizuri kwenye nafasi. Japokuwa hana ufanisi mkubwa kwenye mipira ya mbali, mchango wake kwenye safu ya ulinzi na mashambulizi ya haraka unaleta matokeo chanya kikosini.
ALEX CARUSO
Caruso ni moja ya usajili bora ilioufanya Oklahoma City Thunder msimu huu. Katika msimu wa kawaida, alicheza chini ya dakika 20 kwa mchezo, lakini sasa kwenye mchujo muda wake umeongezeka. Kwenye timu bora zaidi kwa ulinzi msimu huu, Caruso ndiye anapewa jukumu la kumkaba mchezaji wa timu pinzani. Alifungua raundi ya pili dhidi ya Denver Nuggets alama 20, asisti sita na kupokonya mipira mara tano.
JOSH HART
Hart amecheza mechi tatu zilizofuatana na kufunga katika muda muhimu New York Knicks. Licha ya kuwa na urefu wa futi 6 na inchi 4 anapigania rebound dhidi ya wachezaji warefu. Kocha Tom Thibodeau hamwachi benchi dakika za mwisho za mchezo kwa sababu anajua ni mtetezi mwenye msimamo na mtu wa kupigania mipira inayopotea.
BUDDY HIELD
Katika timu ya Golden State Warriors iliyowahi kutegemea mastaa kama Stephen Curry na Klay Thompson, lakini Hield ameibuka kuwa mhimili mpya. Alianza msimu vizuri lakini akapwaya katikati ingawa katika mechi za mchujo amerejea na moto.
Katika mchezo wa mwisho wa raundi ya kwanza dhidi ya Houston Rockets alifunga alama 33 na hakupoteza mpira hata mmoja. Kwa sasa akiwa na nafasi kubwa ya kucheza kutokana na Stephen Curry kuumia, uwezo wake wa kufunga pointi tatu (3-pointers) unaiokoa Warriors.
AL HORFORD
Pamoja na umri kumtupa mkono, Horford bado ni mchezaji mwenye mchango mkubwa Boston Celtics. Ana uwezo wa kushuti mbali na ulinzi bora dhidi ya wachezaji kama Karl-Anthony Towns. Kwa Kristaps Porzingis kuumia mara kwa mara, Celtics wanamhitaji Horford kwa kila hali kuhakikisha wanalinda safu ya chini akiwa anacheza dakika 32 kwa mchezo si haba kwa mchezaji wa miaka 38.
JADEN MCDANIELS
Wengi wanamfahamu McDaniels kwa ulinzi wa kiwango cha juu akiwa na Minnesota Timberwolves. Hata hivyo, katika mchujo ameanza pia kung’ara upande wa mashambulizi. Aliwaumiza Los Angeles Lakers katika mechi mbili kwa pointi 30 na 25 mtawalia - akiwa na asilimia kubwa ya mafanikio kwenye mashuti. Katika kila safari ya mafanikio wapo mashujaa ambao hawatajwi mara kwa mara lakini huacha alama isiyofutika.