Sven-Goran Eriksson afariki dunia siku sita baada ya kuaga
Muktasari:
- Eriksson amefariki baada ya kuugua ugonjwa wa kansa kwa muda mrefu na wikiendi iliyopita aliwaaga watu wa soka na kuwaambia kuwa anakaribia kufariki ikiwa ni miezi michache tangu aliposema kuwa huu ni mwaka wake wa mwisho wa kuishi.
Kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya England na Mancheter City Sven-Goran Eriksson, amefariki dunia akiwa na miaka 76.
Eriksson amefariki baada ya kuugua ugonjwa wa kansa kwa muda mrefu na wikiendi iliyopita aliwaaga watu wa soka na kuwaambia kuwa anakaribia kufariki ikiwa ni miezi michache tangu aliposema kuwa huu ni mwaka wake wa mwisho wa kuishi.
Kocha huyo ambaye aliifundisha timu ya Taifa ya England kwa miaka mitano na kuifikisha kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia alikuwa mmoja kati ya wale wenye heshima kubwa duniani.
Familia yake iliyopo Sweden imetoa taarifa ya kufariki kwa kocha huyo na kusema ni pigo kubwa zaidi kwao.
"Sven-Goran Eriksson amefariki dunia, baada ya kuugua kwa muda mrefu. SGE amefariki leo asubuhi akiwa amezungukwa na familia yake, hili ni pigo kwetu." Imesema taarifa ya familia.
Kocha huyo alikuwa mtu wa kwanza kutoka nje ya England kuifundisha timu hiyo ya taifa mwaka 2001, akiwafundisha mastaa kama David Beckham, Steven Gerrard, Wayne Rooney na Frank Lampard.
Eriksson ambaye alijiuzulu kuifundisha England mwaka 2006, alifanikiwa pia kufundisha timu kadhaa kubwa zikiwemo Leicester City, Manchester City, timu ya Taifa ya Ivory Coast, Benfica na Roma.
Akiwa mkurugenz wa ufundi wa Karlstad ya nchini Sweden mwaka 2023 aliachia ngazi na kutangaza kuwa afya yake haipo vizuri.
Mara ya mwisho alionekana uwanjani wakati alipopewa heshima ya Liverpool ya kuisimamia timu ya wakongwe ya klabu hiyo ilipoivaana na Ajax kwenye Uwanja wa Anfield, Machi mwaka huu.