Suarez amwaga chozi Atletico ikichukua ubingwa

Muktasari:
Ni safari inayokugharimu takriban Sh36,712 kama nauli na dakika 56 kutoka jijini Madrid hadi Jiji la Valladolid kwenye Uwanja wa Estadio Jose Zorrilla kwa treni.
MADRID, HISPANIA. Ni safari inayokugharimu takriban Sh36,712 kama nauli na dakika 56 kutoka jijini Madrid hadi Jiji la Valladolid kwenye Uwanja wa Estadio Jose Zorrilla kwa treni.
Katika safari kwenda katika jiji hilo ilihusisha ‘wahuni’ wanaofundishwa na ‘mhuni’ wa zamani, Diego Simeone maarufu kama El Cholo katika harakati za kufunga pazia la Ligi Kuu Hispania iliyomalizika juzi kwa timu zote kushuka dimbani.
Ndio. Walikuwa ni Atletico Madrid walioandika historia mpya ya kushinda taji la ligi hiyo kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2013/14 ambao unakumbukwa kama msimu wa mshambuliaji mkongwe Diego Costa aliowika sana.
Safari hii Atletico walikwenda kuivaa Real Valladolid wakihitaji matokeo ya ushindi ili kuchukua ubingwa wakati huo Valladolid ilihitaji kushinda na kuiombea mabaya Elche ili kuendelea kusalia kwenye La Liga kwa msimu ujao.
Atletico ilishuka katika mchezo huo ikiwa na tofauti ya alama mbili na waliokuwa wapinzani wao kwenye harakati za kusaka ubingwa, Real Madrid waliokuwa wanacheza mechi ya mwisho dhidi ya Villarreal, na wakashinda kwa mabao 2-1.
Mambo yalianza vibaya kwa Atletico baada ya Valladolid kujipatia bao la kuongoza katika dakika ya 18 kupitia kwa Oscar Plano, lakini mabingwa hao wapya walihitaji dakika 10 kujihakikishia ubingwa kwa mabao ya Angel Correa na Luis Suarez.
Lakini mbali na tukio hilo la kuchukua ubingwa, habari kubwa imekuwa ni Suarez ambaye alimwaga chozi baada ya mechi kumalizika, hali iliyoamsha hisia tofauti kutoka kwa mashabiki na watamazaji.
Itakumbukwa kwamba, kabla ya kuhamia Atletico, mshambuliaji huyo wa zamani wa Liverpool ya England alikuwa katika timu ya Barcelona ambako alitupiwa virago mwishoni mwa msimu uliopita na kutua zake kwa El Cholo.
Katika mahojiano baada ya mchezo, Suarez alisema: “Barcelona haikunipa thamani, lakini Atletico ilifungua milango kwa ajili yangu, kila siku najisikia furaha kwa kile ambacho timu hii imenifanyia, najua Lionel Messi atakuwa na furaha nami kama rafiki yake.
“Lilikuwa ni jambo gumu kukubaliana nalo jinsi Barca ilivyoniondoa, Atletico ilianza vizuri msimu, licha ya changamoto zilizotokea katikati, lakini haikuwa sababu ya kushindwa kwani mwisho wa siku tumeibuka mabingwa.”
Suarez aliuzwa na Barcelona katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi mara baada ya Kocha Ronald Koeman kutua katika kikosi hicho jambo lililowashtua watu wengi ikiwa ni pamoja na Suarez mwenyewe, aliyemwaga chozi kwenye mkutano wa waandishi wa habari wakati akiiaga timu hiyo aliyoipenda.
Baada ya mechi kocha El Cholo alisema wachezaji walijitoa kuanzia mechi ya kwanza hadi ya mwisho ili kuhakikisha kwamba timu hiyo inachukua ubingwa msimu huu.
Akimzungumzia Suarez, Simeone alisema: “Nilisema siku chache zilizopita kwamba huenda ana bahati au mimi nina bahati kwa kuwa naye kwenye timu.”
Msimu huu Suarez amefunga mabao 21.