Arsenal yampa Lewis-Skelly dili

Muktasari:
- Kinda huyo amekubali mkataba mpya wa miaka mitano na hivyo kuvuta kabisa ndoto za Madrid iliyokuwa ikijaribu kumshawishi agomee dili jipya ili akajiunge bure huko Bernabeu.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imejiondoa kwenye presha ya kumpoteza staa wao Myles Lewis-Skelly, ambaye alikuwa kwenye rada za Real Madrid baada ya kumsainisha dili jipya la kumbakiza Emirates.
Kinda huyo amekubali mkataba mpya wa miaka mitano na hivyo kuvuta kabisa ndoto za Madrid iliyokuwa ikijaribu kumshawishi agomee dili jipya ili akajiunge bure huko Bernabeu.
Lewis-Skelly, 18, alikuwa amebakiza mwaka mmoja tu kwenye mkataba wake wa awali, unaomshuhudia akilipwa Pauni 4,000 kwa wiki.
Lakini, Arsenal imeshinda vita ya kumbakiza kinda wao huyo zao la akademia ya Hale End Academy, kwa kumsainisha dili jipya, ambalo limeboresha pia mshahara wake na kuwa mmoja wa makinda wanaolipwa vizuri kwenye soka la dunia.
Lewis-Skelly, ambaye mama yake, mrembo Marcia ndiye aliyesimamia dili hilo, alisema: “Najivunia na nina furaha sana. Nafahamu maneno hayo ni mepesi, lakini yanaelezea hisia zangu za furaha kubwa ya kusaini kwenye klabu hii. Mimi ni shabiki na hii ni kama ndoto iliyotimia.”
Licha ya kwamba alikuwa akicheza kama kiungo kwenye timu za vijana za Arsenal, kocha Mikel Arteta amembadilisha na kumtumia kwenye beki ya kushoto, eneo ambalo amelifanyia kazi nzuri na kuzivutia klabu kama Real Madrid kuhitaji saini yake.