Steven Gerrard ampa ushauri Slot
Muktasari:
- Liverpool ilikuwa imeanza kurejea katika ubora wao siku za karibuni, wakishinda mechi nne mfululizo lakini furaha yao ilikatishwa katika uwanja wa Molineux, baada ya kichapo cha Wolves.
LIVERPOOL, ENGLAND: LEJENDI wa Liverpool, Steven Gerrard ameweka shinikizo kwa Kocha Arne Slot baada ya mwenendo mbaya wa timu hiyo ikiwemo kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Wolves Jumanne usiku.
Liverpool ilikuwa imeanza kurejea katika ubora wao siku za karibuni, wakishinda mechi nne mfululizo lakini furaha yao ilikatishwa katika uwanja wa Molineux, baada ya kichapo cha Wolves.
Akifanya mahojiano na TNT, gwiji huyo wa Liverpool alimhimiza kocha huyo Mholanzi kumwingiza kinda wa miaka 17 Rio Ngumoha katika kikosi cha kwanza, katika mechi ya FA Cup itakayopigwa leo, Ijumaa.
“Kwa dakika 65 Liverpool walikuwa hoi kabisa usiku huu, walicheza vibaya sana, hawakutengeneza nafasi za kutosha, hawakucheza kwa kasi na mpangilio sahihi. Hawakuwa na ubora kabisa, lazima amuanzishe Ngumoha sasa. Lazima aanze kwa sababu anaingia kama mchezaji wa akiba na anafanya mengi zaidi kwa muda mfupi kuliko anavyofanya Cody Gakpo katika dakika 65–70. Anastahili kuanza sasa."
Ngumoha aliyefunga bao la ushindi katika dakika za mwisho dhidi ya Newcastle United mapema msimu huu, amekuwa akitokea benchi katika mechi tatu za mwisho za Liverpool kwenye Ligi Kuu England.
Katika mechi zake 17 alizocheza, alianza kikosi cha kwanza kwenye mechi mbili tu, dhidi ya Crystal Palace na Barnsley zilizopigwa Uwanja wa Anfield.