Pambano la Fury, Joshua lazua utata
Muktasari:
- Kauli hiyo imekuja wakati kukiwa na tetesi zinazodai pambano hilo la uzani wa juu linaweza kufanyika jijini Las Vegas, Marekani, badala ya Uingereza kama ilivyopangwa awali.
LONDON, ENGLAND: PROMOTA wa bondia Anthony Joshua, Eddie Hearn amesema pambano kubwa linalosubiriwa kwa hamu kati ya Anthony Joshua na Tyson Fury limepangwa kufanyika Uingereza na litahamishiwa Marekani ikiwa kutafikiwa makubaliano mapya kati ya pande husika.
Kauli hiyo imekuja wakati kukiwa na tetesi zinazodai pambano hilo la uzani wa juu linaweza kufanyika jijini Las Vegas, Marekani, badala ya Uingereza kama ilivyopangwa awali.
Hearn, ambaye amekuwa akimsimamia Joshua tangu alipoingia katika mchezo wa ngumi za kulipwa mwaka 2013, amesema mkataba wa sasa unaeleza wazi pambano hilo ni la kufanyika Uingereza na mabadiliko yoyote yatahitaji mazungumzo mapya.
“Tuna uhusiano mzuri sana na Turki Alalshikh. Kama atakuja na kutuambia anataka pambano lifanyike Marekani kwa sababu fulani, bila shaka tutasikitika kwa sababu naamini kila mtu anafikiri pambano hili linapaswa kufanyika Uingereza,” amesema Hearn.
Hata hivyo, Hearn alikiri kutokana na gharama kubwa za kuandaa pambano hilo, kuna uwezekano wa kufanya marekebisho endapo waandaaji wataona kuna ulazima wa kufanya hivyo.
“Analipa gharama zote na gharama hizo ni kubwa sana. Kama wanataka kubadilisha chochote katika mkataba, basi tutalazimika kuanza mazungumzo mapya,” ameongeza.
Mbali na hilo, Hearn alipinga madai ya rais wa UFC, Dana White, kampuni yake ya Zuffa Boxing itahusika katika kuandaa pambano hilo.
Kwa mujibu wa Hearn, Zuffa Boxing haina nafasi yoyote kwa sasa katika maandalizi ya pambano hilo isipokuwa kama upande wa Joshua utakubali kufanya mabadiliko ya mkataba.
Awali, promota wa Tyson Fury, Frank Warren amesema kutakuwa na kikao kati ya waandaaji mbalimbali wiki ijayo ili kujadili tarehe na eneo rasmi la pambano hilo.
Hearn amesema anatarajia kikao hicho kufanyika kama ilivyopangwa, huku akisisitiza ana imani kubwa pambano hilo litafanyika mwaka huu.
Hata hivyo, ameeleza jambo pekee linaloweza kuzuia pambano hilo ni iwapo Joshua atashindwa katika pambano lake dhidi ya Kristian Prenga litakalofanyika Julai 25 au Fury akapoteza pambano lake la mpito linalotarajiwa kufanyika Agosti 1.
“Nina uhakika kwa asilimia 100 pambano hili litafanyika mwaka 2026 isipokuwa mmoja wao atashindwa pambano lake la maandalizi,” amesema Hearn.
Pambano kati ya Joshua na Fury limekuwa likisubiriwa kwa muda mrefu na mashabiki wa ngumi duniani, huku wengi wakilitaja kuwa moja ya mapambano makubwa zaidi kuwahi kukutanisha mabondia wa Uingereza.