Steven Gerrard aikosoa Liverpool baada ya kipigo cha Wolves
Muktasari:
- Liverpool imepoteza kwa bao la dakika za mwishoni ugenini dhidi ya Wolves, matokeo yaliyotikisa matumaini yao ya kumaliza ndani ya nne bora na kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
MOLINEUX, ENGLAND. Nguli wa zamani wa Liverpool, Steven Gerrard, ameikosoa vikali klabu yake hiyo kufuatia kipigo cha mabao 2-1 walichopata dhidi ya Wolves katika mechi ya Ligi Kuu England iliyopigwa jana usiku, akieleza kuwa walicheza kwa kiwango cha chini na kukosa ubora unaotakiwa.
Liverpool imepoteza kwa bao la dakika za mwishoni ugenini dhidi ya Wolves, matokeo yaliyotikisa matumaini yao ya kumaliza ndani ya nne bora na kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Akizungumza baada ya mchezo Gerrard amesema:
“Kwa dakika 65, Liverpool walikuwa wa hovyo kabisa. Hawakuwa na kasi sahihi wala ubora.”
Gerrard pia amemtaka kocha Arne Slot kumpa nafasi mshambuliaji chipukizi Rio Ngumoha, akidai ana mchango mkubwa zaidi kuliko baadhi ya wachezaji waliocheza muda mrefu.
“Anachokifanya kwa dakika chache ni zaidi ya alichofanya Cody Gakpo ndani ya dakika 65. Anastahili kuanza. Kocha lazima aanze naye,” amesema.
Msimu huu, Liverpool imepoteza michezo mitano kwa mabao ya dakika za majeruhi, idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea kwao ndani ya msimu mmoja wa Ligi Kuu England.
Akizungumzia mabao waliyofungwa, Gerrard ameilaumu safu ya ulinzi akisema bao la kwanza lilitokana na uzembe wa kawaida.
“Ilikuwa pasi rahisi kwenda kwa mshambuliaji, kulikuwa na wachezaji wawili dhidi ya mmoja, hilo lilipaswa kuzuiwa,” amesema.
Kwa bao la pili, amemlaumu kipa Alisson Becker kwa kupiga mpira mbovu ulioanzisha shambulio, huku akisema hakukuwa na mwitikio wa haraka kutoka kwa mabeki.
Aidha, Gerrard hakukubaliana na madai ya baadhi ya mashabiki waliodai kuwa kulikuwa na faulo dhidi ya nahodha, Virgil van Dijk kabla ya bao la kwanza.
“Sidhani kama ilikuwa faulo. Anatakiwa awe imara zaidi katika mazingira kama yale,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Van Dijk amekiri timu ilicheza chini ya kiwango.
“Ilikuwa taratibu, tulikuwa rahisi kutabirika na tulifanya maamuzi mabovu,” amesema nahodha huyo baada ya mchezo.
Kipigo hicho kimeiweka Liverpool katika hali tete kwenye mbio za kumaliza ndani ya tano bora. Endapo Chelsea watashinda mechi yao inayofuata dhidi ya Aston Villa, wanaweza kuipiku Liverpool kutokana na tofauti ya mabao.
Hata hivyo, Liverpool wana nafasi ya kulipa kisasi watakaporejea Molineux kwa mchezo wa Kombe la FA kabla ya kurejea Anfield kuikaribisha Tottenham katika Ligi Kuu.