Slot aomba ufafanuzi penalti ya Man United
Muktasari:
- Beki wa Crystal Palace, Lacroix, alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kusababisha penalti, hatua iliyochochea Manchester United kurejea na kushinda mabao 2-1 uwanjani Old Trafford, Jumapili.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot, ameitaka Ligi Kuu England kutoa ufafanuzi kuhusu kutokuwapo kwa uwiano katika maamuzi muhimu ya waamuzi, baada ya kulinganisha kadi nyekundu aliyoonyeshwa Maxence Lacroix wa Crystal Palace na tukio la Marc Guehi kumvuta jezi Mohamed Salah katika mechi ya mwezi uliopita.
Beki wa Crystal Palace, Lacroix, alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kusababisha penalti, hatua iliyochochea Manchester United kurejea na kushinda mabao 2-1 uwanjani Old Trafford, Jumapili.
Slot alizungumzia mjadala huo katika mkutano wake na waandishi wa habari, Jumatatu, baada ya baadhi kuhoji uamuzi wa mwamuzi Chris Kavanagh kutoa penalti na kadi nyekundu. Miongoni mwa waliokosoa ni Gary Lineker ambaye aliita adhabu hiyo kuwa kali kupita kiasi.
Kocha huyo wa Liverpool alikumbusha tukio la awali msimu huu ambapo Guehi alimvuta Salah alipokuwa akielekea golini. Katika tukio hilo, Guehi alionyeshwa kadi ya njano na Liverpool ikapewa mpira wa adhabu, huku VAR ikiunga mkono uamuzi wa mwamuzi wa uwanjani.
Hata hivyo, katika mechi dhidi ya Man United, VAR iliingilia kati na kushauri Lacroix aonyeshwe kadi nyekundu, licha ya mwamuzi kutotoa kadi awali. Slot anaamini matukio yote mawili yalistahili kadi nyekundu na akasisitiza Ligi Kuu England inapaswa kukiri makosa yanapotokea.
“Nikiangalia matukio hayo, naona umbali unaofanana. Labda hata umbali kati ya Guehi na mchezaji aliyekuwa karibu ulikuwa mkubwa zaidi kuliko ule wa mabeki wa Palace katika tukio la Lacroix. Mara ya kwanza nilipoona tukio hilo, nikikumbuka kilichotokea kwetu, nilidhani VAR ingeangalia kama ni penalti au kama tukio lilikuwa ndani au nje ya eneo, lakini si kutoa kadi nyekundu,” alisema Slot.
“Hapa ndipo ninapokuwa na tatizo na VAR. Kila mara Ligi Kuu England wanasema kulikuwa na maamuzi mawili tu mabaya msimu mzima, lakini katika matukio kama haya unatarajia VAR iingilie kati. Mara tisa kati ya kumi katika soka, kuna tofauti kati ya ‘mwamuzi ametoa kadi nyekundu na ninaheshimu uamuzi wake’ au ‘mwamuzi hajatoa kadi nyekundu na ninaheshimu uamuzi wake’.
“Lakini hapa, katika matukio yote mawili, mwamuzi hakutoa kadi nyekundu ila katika moja VAR ikaingilia na kubadili uamuzi. Kwangu, moja kati ya hayo ni kosa.”