Stanley Nwabali hatarini kutemwa Super Eagles
Muktasari:
- Nigeria inatarajia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Irani Machi 27, 2026 na siku tatu baadae itapambana na Jordan.
KOCHA wa timu ya taifa ya Nigeria, Eric Chelle, huenda akamtema kipa Stanley Nwabali kwenye kikosi cha Super Eagles kitakachocheza mechi mbili za kimataifa za kirafiki Machi 2026.
Nigeria inatarajia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Irani Machi 27, 2026 na siku tatu baadae itapambana na Jordan.
Taarifa zinaeleza kuwa, Kocha Chelle anajipanga kumwacha Nwabali, kutokana na kukosa klabu kwa sasa, baada ya kuachana na Chippa United mwanzoni mwa mwezi huu, huku akihusishwa na mpango wa kusajiliwa na klabu za Tanzania na Marekani, lakini hakuna makubaliano yoyote rasmi yaliyofikiwa.
Kocha chelle anahisi huenda uwezo wa kipa huyo ukawa umeshuka kutokana na kukosa baadhi ya mechi kwa sasa, hivyo anajipanga kumtangaza kipa mwingine ambaye atakuwa na sifa ya kucheza mara kwa mara katika klabu yake.
Kutokana na hilo, kipa Arthur Okonkwo, ambaye kwa mujibu wa ripoti amepata kibali cha FIFA cha kubadilisha uraia kutoka England na kuwa Mnigeria. Kipa huyo wa miaka 24, alikuzwa katika kituo cha mafunzo chaa Arsenal, anadaiwa kuthibitisha kujitolea kwake katika kikosi cha Super Eagles.
Kwa mara ya kwanza Nigeria itacheza mechi hizo za kimataifa za kirafiki, baada AFCON 2025 ambapo ilishuhudia nchi hiyo ikimaliza nafasi ya tatu kwa kuifunga Misri 1-0.
Katika michuano ya AFCON 2025, Nigeria ilionyesha uwezo mkubwa baada ya kucheza mechi saba, ikipata ushindi mara sita na sare moja ya kawaida ndani ya dakika 90. Ushindi huo umeifanya Super Eagles kutopoteza mechi yoyote ndani ya muda wa kawaida, huku suluhu dhidi ya wenyeji Morocco hatua ya nusu fainali ikiamuliwa na changamoto ya mikwaju ya penalti.
Katika mashindano hayo, Nigeria imeonekana kuwa timu yenye nguvu kubwa ya ushambuliaji, ikifunga jumla ya mabao 14, zaidi ya timu nyingine yoyote iliyoshiriki AFCON 2025.
Baada ya matokeo hayo mazuri kwenye AFCON 2025, Nigeria imepanda hadi nafasi ya 26 katika orodha ya viwango vya ubora vya soka duniani, ikiendelea kuwa moja ya timu bora barani Afrika, ikishika nafasi ya 3 Afrika.