Kichapo cha DR Congo bado kinamuuma Stanley Nwabali
Muktasari:
- Miamba hiyo ya Afrika ilimaliza dakika 120 kwa sare ya bao 1-1 baada ya mechi iliyokuwa imejaa matumizi makubwa ya nguvu kwa wachezaji wa pande zote mbili ambao walionyesha kuhitaji matokeo ya ushindi.
Kipa wa timu ya taifa ya Nigeria, Stanley Nwabali amekiri kuumizwa na matokeo ya mechi ya mwisho ya kufuzu Kombe la Dunia 2026, ambayo alishuhudia wakichapwa kwa penalti 4-3 dhidi ya DR Congo, usiku wa kuamkia leo Jumatatu, Novemba 17, 2025.
Miamba hiyo ya Afrika ilimaliza dakika 120 kwa sare ya bao 1-1 baada ya mechi iliyokuwa imejaa matumizi makubwa ya nguvu kwa wachezaji wa pande zote mbili ambao walionyesha kuhitaji matokeo ya ushindi.
Nwabali ametumia mtandao wa Instagram kuonyesha hisia za maumivu, kwa kuandika ujumbe mzito kufuatia kichapo hicho.
"Ni matokeo ya kuumiza! Sote tulijitahidi kwa ajili ya nembo ya timu ya taifa, ingawa juhudi zetu hazikutosha. Niliwahi kuwa shabiki na ninaelewa jinsi inavyoumiza, matokeo haya tunayachukua kama sehemu ya uwajibikaji wetu kama wachezaji,” ameandika kipa huyo wa klabu ya Chippa United ya Afrika Kusini.
Safari ya Nigeria ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 ilikuwa yenye misukosuko na matumaini ambayo hatimaye imekatishwa na DR Congo.
Katika hatua ya makundi ya mchujo ukanda wa Afrika, Nigeria ilikuwa Kundi C na kumaliza ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Afrika Kusini. Ingawa haikufuzu moja kwa moja kama mabingwa wa kundi, nafasi yao kama moja ya timu bora zilizomaliza nafasi ya pili iliwafanya iingie kwenye hatua ya mchujo maalumu (CAF play-offs).
Katika hatua hiyo, Nigeria ilianza vyema kwa kuifunga Gabon 4–1 kwenye nusu fainali baada ya mechi kwenda muda wa ziada, hivyo kufuzu kucheza fainali ya mchujo dhidi ya DR Congo.
Fainali hiyo ilichezwa mjini Rabat, Morocco, Nigeria ilianza kwa nguvu kwa kufunga bao la mapema kupitia Frank Onyeka. Hata hivyo, DR Congo ilirejea mchezoni na kusawazisha kupitia Meschack Elia, na mechi ikamalizika 1–1 baada ya dakika 120.
Hatma ya Super Eagles ikaamuliwa kupitia mikwaju ya penalti, ambapo DR Congo ilishinda 4–3. Kwa matokeo hayo, Nigeria imeondolewa kwenye mbio za kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya pili mfululizo, na safari yao ya kuelekea 2026 ikafikia kikomo kwa njia ya kusikitisha licha ya juhudi kubwa za kikosi hicho.