Spurs kujipanga upya, yamwaga pesa
Muktasari:
- Spurs ilitangaza Alhamisi ya wiki iliyopita Levy ameondoka baada ya kuhudumu kwa karibu miaka 25 madarakani.
LONDON, ENGLAND: WAMILIKI wa Tottenham kampuni ya ENIC, wako tayari kuwekeza Pauni 100 milioni katika klabu hiyo ikiwa ni siku kadhaa baada ya kuachana na mwenyekiti Daniel Levy.
Spurs ilitangaza Alhamisi ya wiki iliyopita Levy ameondoka baada ya kuhudumu kwa karibu miaka 25 madarakani.
Hata hivyo, ripoti nyingi zimeeleza wamiliki wa klabu, ENIC wakiongozwa na mfanyabiashara wa Uingereza, Joe Lewis waliamua kumwondoa Levy na wala hakujizulu kwa kupenda.
Kwa mujibu wa ripoti mpya kutoka tovuti ya The Telegraph, inafahamika uamuzi wa kumwondoa Levy ni sehemu ya mkakati mpya wa ENIC kusaidia Tottenham kujenga mafanikio baada ya ushindi wa taji la Europa League Mei mwaka huu ambalo lilikuwa ni kombe la kwanza la klabu hiyo katika miaka 17. Ripoti hiyo inaeleza ENIC na Lewis hawana nia ya kuuza klabu, hivyo wanataka kuwekeza zaidi ili kuhakikisha timu inaongeza ushindani na kupambana vilivyo sokoni kupata wachezaji bora watakaowawezesha kushindana na vigogo kama Liverpool, Manchester City, Chelsea na mahasimu wao wa karibu, Arsenal.
Tottenham ilitumia zaidi ya Pauni 150 milioni dirisha lililopita la majira ya kiangazi ili kusajili ambao Kocha Thomas Frank aliwahitaji.
Klabu hiyo yenye maskani yake Kaskazini mwa Jiji la London ilimsajili Xavi Simons kutoka RB Leipzig na Mohamed Kudus kutoka West Ham United.
Pia iliwasainisha mikataba ya muda mrefu Mathys Tel na Kevin Danso baada ya kuvutiwa na kiwango walichoonyesha walipokuwa wakicheza kwa mkopo katika timu hiyo msimu uliopita.
Spurs pia iliwasajili kwa mkopo kiungo wa Bayern Munich, Joao Palhinha, na mshambuliaji wa Paris Saint-Germain, Randal Kolo Muani.
Tottenham itakuwa na mechi ugenini dhidi ya majirani zao wa London, West Ham, katika Ligi Kuu England, Septemba 13.