Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Olise atikisa kiberiti Bayern

Muktasari:

  • Nyota huyo wa Ufaransa, ambaye alijiunga na Bayern Munich akitokea Crystal Palace mwaka 2024, anataka kufafanua mustakabali wake ndani ya klabu hiyo.

MADRID, Hispania: MSHAMBULIAJI Michael Olise ameripotiwa kuomba kikao na viongozi wa Bayern Munich huku tetesi za uhamisho wake zikiendelea kushika kasi.

Nyota huyo wa Ufaransa, ambaye alijiunga na Bayern Munich akitokea Crystal Palace mwaka 2024, anataka kufafanua mustakabali wake ndani ya klabu hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti la AS, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 anataka kuondoa sintofahamu na kujua nafasi yake ndani ya Bayern baada ya msimu bora aliouonyesha.

Kikao hicho kitawapa viongozi wa Bayern fursa ya kwanza kujua mawazo ya Olise, huku wakihofia kuwa tetesi zinazoendelea kuhusu uhamisho wake huenda zimeanza kumshawishi kufikiria kuondoka.

Wakati huo huo, Real Madrid inadaiwa kufuatilia kwa karibu maendeleo hayo huku ikijiandaa kutoa ofa kubwa ya pauni191 milioni ili kumsajili nyota huyo.

Rais wa klabu hiyo, Florentino Perez ambaye hivi karibuni alichaguliwa kwa muhula wake wa nane na kuongeza muda wake wa uongozi hadi mwaka 2030, anadaiwa kumwona Olise kama usajili wake wa ndoto.

Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Hispania Marca, mabingwa hao wa Ulaya mara 15 wanaweza kutoa takribani pauni190 milioni ili kuishawishi Bayern Munich kumuuza.

Inaaminika pia kuwa Olise anaweza kuungana tena na mwenzake wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe, katika kikosi cha Real Madrid kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.

Olise pia anaonekana kuwa chaguo kuu la muda mrefu la Real Madrid endapo mazungumzo ya kuongeza mkataba wa Vinicius Junior yatashindikana kabisa.

Katika Kombe la Dunia, Olise alitoa pasi ya bao la kwanza la Mbappe wakati Ufaransa ilipoifunga Senegal mabao 3-1 katika mchezo wao wa ufunguzi.

Wakati nyota huyo akiwa na timu ya taifa, klabu mbalimbali za Ulaya zimeendelea kufuatilia kwa karibu hali yake ndani ya Bayern ili kujua hatua atakazochukua baada ya mashindano hayo.

Lengo la kikao hicho na Bayern ni kuchambua hali yake, kujadili mustakabali wake na kupanga hatua zinazofuata baada ya kuzidi matarajio ya wengi tangu alipojiunga na klabu hiyo.

Kwa sasa, Olise ameshatwaa mataji mawili ya Bundesliga, pamoja na Kombe la Ujerumani na Super Cup ya Ujerumani akiwa na Bayern Munich.

Msimu uliopita, mchezaji huyo aliyeshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Bundesliga alicheza mechi 52 katika mashindano yote, akifunga mabao 22 na kutoa asisti 31.

Mbali na Real Madrid, Paris Saint-Germain pamoja na baadhi ya klabu za Ligi Kuu England pia zinadaiwa kuvutiwa na huduma zake.

Dirisha la usajili la Bundesliga limefunguliwa jana Julai 1 na litafungwa Agosti 31.