Rungu la Uefa lazipitia tatu EPL
Muktasari:
- Taarifa zinasema Newcastle United, Chelsea na Aston Villa zimepigwa faini kwa kukiuka kanuni za kifedha za Uefa, ambapo zote tatu zilishiriki mashindano ya Ulaya msimu uliomalizika.
NYON, USWISI: RUNGU la Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) limezishukia timu tatu za Ligi Kuu England (EPL), likizituhumu kukiuka kanuni za matumizi ya kifedha katika masuala mbalimbali ya uendeshaji.
Taarifa zinasema Newcastle United, Chelsea na Aston Villa zimepigwa faini kwa kukiuka kanuni za kifedha za Uefa, ambapo zote tatu zilishiriki mashindano ya Ulaya msimu uliomalizika.
Newcastle ilishiriki Ligi ya Mabingwa sambamba na Chelsea huku Aton Villa ikikipiga katika michuano ya Europa League ambapo ilibeba ubingwa wa mashindano hayo.
Kwa mujibu wa taarifa Newcastle United imepigwa faini ya Euro 6 milioni baada ya kukiuka kanuni za uendelevu wa kifedha za shirikisho hilo, huku Aston Villa na Chelsea zikiadhibiwa kwa kutumia fedha kupita kiwango kinachoruhusiwa kwa mwaka wa pili mfululizo.
Inaelezwa kwamba baada ya uchunguzi uliofanywa na Kitengo cha Udhibiti wa Fedha za Klabu cha UEFA (CFCB), Newcastle ilibainika kukiuka Kanuni ya Mapato ya Soka (FER) pamoja na ile ya gharama za kikosi (SCR) na kwamba kila kosa lilisababisha faini ya Euro 3 milioni, huku Euro 7 milioni nyingine zikisimamishwa na zitalipwa endapo klabu hiyo itakiuka tena kanuni hizo katika siku zijazo.
Ingawa Newcastle United haijafuzu kushiriki mashindano ya Ulaya msimu ujao baada ya kumaliza katika nafasi ya 10 kwenye Ligi Kuu England, ilifika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika kipindi kilichofanyiwa tathmini, hivyo iliwajibika kufuata kanuni za kifedha za Uefa.
Klabu hiyo haijawahi kukiuka Kanuni za Faida na Uendelevu (PSR) za Ligi Kuu England, ambazo zinatarajiwa kubadilishwa na mfumo unaofanana na SCR kuanzia msimu ujao. Hata hivyo, kanuni za Uefa ni kali zaidi.
Kwa mujibu wa shirikisho hilo, klabu zinatakiwa kutumia siyo zaidi ya asilimia 70 ya mapato kwa ajili ya mishahara ya wachezaji na gharama nyingine za kikosi, tofauti na Ligi Kuu England inayoruhusu hadi asilimia 85. Pia, chini ya FER, klabu haziruhusiwi kuongeza mapato kupitia uuzaji wa mali inazomiliki.
Inaelezwa kuwa Newcastle United ilitumia takriban asilimia 75 ya mapato yake kwa gharama za kikosi msimu uliopita.
Pia, Uefa haikukubali uuzaji wa Uwanja wa St James' Park kwa kampuni tanzu ya PZ Newco Holdings kama sehemu ya mapato yanayoweza kuhesabiwa katika taarifa za kifedha.
Katika taarifa yake, Newcastle ilisema: "Newcastle United imeingia makubaliano ya suluhu na Uefa baada ya kukiuka kanuni za uendelevu wa kifedha katika kipindi cha miaka mitatu kilichoishia Juni 2025. Kufuatia matumizi yaliyovuka kiwango kinachoruhusiwa chini ya Kanuni ya Mapato ya Soka, klabu imefanya kazi kwa karibu na kwa ushirikiano na Kitengo cha Udhibiti wa Fedha za Klabu ili kutatua suala hili haraka."
Klabu hiyo iliongeza kuwa imekubali makubaliano ya miaka mitatu yanayojumuisha faini ya Euro 3 milioni 3, huku Euro 7 milioni zikisubiri kulipwa iwapo itashindwa kuzingatia kanuni hizo siku zijazo. Pia, italipa Euro 3 milioni nyingine baada ya kukiuka kiwango cha asilimia 70 cha matumizi ya kikosi kwa mwaka wa kalenda wa 2025.
Newcastle United imesema inaishukuru UEFA kwa namna ilivyoshughulikia suala hilo na imejizatiti kuhakikisha inafuata kikamilifu kanuni zote za kifedha kuanzia sasa. Adhabu hiyo inaonyesha kuwa, licha ya Newcastle kumilikiwa na Saudi Arabia Public Investment Fund (PIF) yenye uwezo mkubwa kifedha, bado inalazimika kuheshimu kanuni za matumizi za Uefa.
Klabu ilisema faini hiyo haitabadilisha mipango yake katika usajili wa wachezaji msimu huu wa kiangazi. Hata hivyo, tayari imemuuza Anthony Gordon kwenda Barcelona kwa Pauni 75 milioni, huku kiungo Sandro Tonali akihusishwa kuondoka kwa takriban Pauni 100 milioni kutokana na kuvutiwa na Man City na Tottenham Hotspur.
VILLA, CHELSEA WAGUSWA
Kwa upande mwingine Aston Villa imepigwa faini ya Euro 22.5 milioni kwa kukiuka kiwango cha asilimia 70 cha SCR kwa mwaka wa pili mfululizo. Hata hivyo, italipa Euro 7.5 milioni pekee kwa sasa, huku kiasi kilichobaki kikisimamishwa isipokuwa ikikiuka tena kanuni hizo.
Villa imefanikiwa kupunguza matumizi yake hadi chini ya asilimia 80 ya kiwango kilichokuwa kimekiukwa awali, baada ya mwaka uliopita kupigwa faini ya Euro 11 milioni.
Nayo Chelsea imeonyesha maendeleo makubwa zaidi katika kupunguza matumizi yake kupita kiwango, jambo lililoifanya kulimwa faini ya Euro 3 milioni pekee, ambapo Euro 2 milioni kati ya hizo zimesimamishwa.
UEFA ilisema: "Kwa Aston Villa na Chelsea, ambazo tayari zilikuwa zimeadhibiwa msimu uliopita, Kitengo cha Udhibiti wa Fedha kilizingatia maendeleo mazuri yaliyofikiwa katika kupunguza uwiano wa gharama za vikosi kati ya 2024 na 2025, kulingana na makadirio yaliyowasilishwa katika makubaliano yao ya awali." Shirikisho hilo liliongeza kuwa sehemu ya faini hizo itategemea uwezo wa klabu hizo kuendelea kupunguza matumizi ya vikosi mwaka 2026.