Southgate apangiwa kikosi, Senegal afe kipa, afe beki

DOHA QATAR. ISHAKUWA soo. England inatafuta namna ya kutinga hatua ya mtoano kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar na jambo hilo linamfanya staa wa zamani wa miamba hiyo, Joe Cole kumtaka Kocha Gareth Southgate kufanya mabadiliko ya wachezaji wanne kwenye kikosi chake kitakachochuana na Wales leo Jumanne, ikiwamo kumpiga chini straika namba moja na nahodha, Harry Kane.

England ilitoka sare ya bila kufungana dhidi ya Marekani kwenye mchezo wa pili wa hatua ya makundi Ijumaa iliyopita baada ya kuanza kampeni kwenye Kombe la Dunia 2022 kwa kishindo cha ushindi wa mabao 6-2 dhidi ya Iran, ambayo ilishinda mechi yake ya pili kwenye Kundi B ilipokipiga na Wales.

England bado inaongoza kwenye Kundi B kwa kukusanya pointi nne, ikifuatiwa na Iran yenye pointi tatu na Marekani kwenye nafasi ya tatu ikiwa na pointi mbili na Wales inashika mkia kwenye kundi hilo ikiwa na pointi moja. Kwa mambo jinsi yalivyo, England bado haipo salama kwenye mpango wake wa kuongoza kundi kama itachapwa na Wales kisha Iran na Marekani yeyote akishinda, basi shughuli itakuwa pevu kwao. Umuhimu wa kuongoza kundi unakwenda kukutana na mbabe wa kundi jingine.

Kuhusu Joe Cole kikosi anachotaka Kocha Southgate aanze nacho, golini kama kawaida ni Jordan Pickford na ukuta wake ulindwe na Harry Maguire, John Stones, Luke Shaw na Kieran Trippier. Kwenye eneo la kiungo ndipo mabadiliko yanapohitaji, ambapo Jordan Henderson akipaswa kuanza sambamba na Declan Rice, huku kwenye Namba 10 acheze Phil Foden, kushoto aanzie Jack Grealish na kulia kama kawaida abaki Bukayo Saka na kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati, Marcus Rashford aanzishwe mbele ya Kane. Cole anaamini mikimbio ya Rashford akicheza mbele ya wakali watatu Saka, Foden na Grealish suala la kufunga mabao halitakuwa na shida na kuamini Kane anahitaji kupumzishwa.

Hiyo ina maana Jude Bellingham, Mason Mount, Raheem Sterling na Kane kuanzia kwenye benchi. Rekodi zinaonyesha, England kwenye mechi zake dhidi ya Wales zimekutana mara sita kwenye michuano tofauti na zote kikosi cha Three Lions kimeibuka na ushindi. Je, Gareth Bale na wenzake wataweza kupindua meza kwenye Kombe la Dunia?

Mchezo mwingine kwenye kundi hilo utakuwa baina ya Iran na Marekani. Miamba hiyo miwili ina uhasama wa kisiasa iliwahi kukutana mara mbili, ikiwamo moja kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Dunia 1998 huko Ufaransa. Kwenye mechi hiyo ya Kombe la Dunia 1998, Iran ilishinda mabao 2-1, huku mechi nyingine ya kirafiki ilimalizika kwa sare ya bao 1-1, ambapo kipute kilipigwa Januari 2000. Mechi yao ya kipindi hiki kwenye fainali hizo za Qatar ina upinzani mkali, kwani yoyote atakayechapwa basi atakuwa amefungasha virago na kutupwa nje ya michuano.

Mechi nyingine za kukamilisha hatua ya makundi ni zile za Kundi A, ambapo kuna vita ya timu tatu, Uholanzi, Senegal na Ecuador katika kusaka tiketi ya kutinga hatua ya 16 bora katika fainali hizo za Kombe la Dunia 2022.

Wenyeji Qatar wamepokea vichapo viwili na kutupwa nje ya michuano na kwamba leo wataingia uwanjani kukamilisha ratiba, watakapokipiga na Uholanzi.

Hata hivyo, mechi hiyo haitakuwa nyepesi kwa Uholanzi kutokana na Qatar kuhitaji walau kushinda au kupata pointi yoyote katika fainali hizo kama waandaaji. Kwa hivyo, patachimbika. Msimamo wa Kundi A ulivyo baada ya mechi mbili, Uholanzi imekusanya pointi nne sawa na Ecuador, huku Senegal ikiwa na pointi tatu na Qatar ina pointi sifuri. Shughuli pevu itakuwe kwenye mechi ya Ecuador na Senegal, ambapo watania nafasi moja ya kutinga hatua inayofuata.

Senegal itahitaji kupata ushindi wa lazima kama inahitaji kusonga mbele, kwani sare haitawasaidia kitu labda kama tu Uholanzi atapoteza kwa idadi kubwa ya mabao inayoanzia 3-0 mbele ya Qatar. Mambo ni moto.