Solskjaer, Man United kuna kitu kinapikwa
Muktasari:
- Man United imewasiliana na Solskjaer pamoja na Michael Carrick kuhusu uwezekano wa kuchukua nafasi ya kocha wa mpito kwa kipindi kilichosalia cha msimu.
MANCHESTER, ENGLAND: OLE Gunnar Solskjaer ameripotiwa kwamba angetumia siku ya jana Jumamosi kufanya mazungumzo zaidi ya kuhusu kibarua cha kuinoa Manchester United.
Man United imewasiliana na Solskjaer pamoja na Michael Carrick kuhusu uwezekano wa kuchukua nafasi ya kocha wa mpito kwa kipindi kilichosalia cha msimu.
Carrick alizungumza na viongozi wa Man United, Alhamisi iliyopita, akiwa likizo Barbados pamoja na aliyekuwa mchezaji mwenzake, Wayne Rooney. Solskjaer, 52, alirejea kuishi Cheshire mwezi Septemba baada ya kufukuzwa kazi na Besiktas.
Raia huyo wa Norway aliwahi kuinoa Man United kati ya mwaka 2018 na 2021.
Katika kipindi chake, aliiongoza Man United kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England.
Kazi ya mwisho ya Carrick katika ukocha ilikuwa Middlesbrough, lakini aliondoka baada ya kushindwa kufuzu kwa michuano ya mtoano ya Championship mwaka jana. Vyanzo vinasema Carrick amekuwa kimya bila kelele nyingi huku Man United wakionyesha ghafla nia baada ya kufukuzwa kwa Ruben Amorim, asubuhi ya Jumatatu iliyopita.
Kiungo huyo wa zamani, mwenye umri wa miaka 44, pia aliwahi kuinoa Man United kwa muda kama kocha wa mpito katika mechi tatu mwaka 2021. Man United iliifunga Villarreal na Arsenal, pamoja na kupata sare dhidi ya Chelsea, wakati Carrick akiwa kocha wa muda.
Kuna pia ulinganisho wa mameneja wa Man United wakiwemo Amorim, Ralf Rangnick, David Moyes, Louis Van Gaal, Ole Gunnar Solskjaer, Erik ten Hag, Jose Mourinho na Alex Ferguson, unaoonyesha idadi ya mechi walizoongoza, ushindi, sare, vipigo na ushindi.
Wakala wa Solskjaer, Jim Solbakken, alitarajiwa kuwepo katika mazungumzo hayo ya Jumamosi. Man United ilimfuta kazi Solskjaer, Novemba 2021 baada ya kupoteza mechi tano kati ya saba za Ligi Kuu. Hata hivyo, baada ya Amorim kumkosoa wazi mkurugenzi wa michezo Jason Wilcox katika kauli ya kushangaza Jumapili, Man United iliamua kumfuta kazi kocha huyo raia wa Ureno ndani ya saa 24.
Kocha wa mpito Darren Fletcher ataendelea kuwaongoza Man United katika mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA dhidi ya Brighton, Jumapili uwanjani Old Trafford.