Slot hataki kushangilia
Muktasari:
- Liverpool imeingia wikiendi hii ikiwa juu ya msimamo wa ligi na katika mechi 11 za michuano ligi imepoteza moja tu.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot amesisitiza timu yake haitobweteka licha ya kuongoza ligi kwani wanaamini Manchester City wanawawinda kimya kimya.
Liverpool imeingia wikiendi hii ikiwa juu ya msimamo wa ligi na katika mechi 11 za michuano ligi imepoteza moja tu.
Kocha huyu ametoa mfano wa miaka miwili iliyopita, Arsenal ilipokuwa inaongoza ligi kwa pointi nane na zilikuwa zimebakia mechi 10 lakini ikapoteza ubingwa mbele ya Man City sawa na Liverpool wenyewe ambao waliwahi kuwa na uongozi wa pointi tatu mbele ya Man City hadi kufikia Aprili na bado ikashindwa kuchukua ubingwa.
Liverpool ambayo itakutana na Southampton kesho, kwa sasa inaongoza kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Man City ambayo ipo nafasi yapili kwa pointi 23.
“Sote tunatambua tumecheza mechi 11 za msimu na hatutajivunia hilo au kuanza kusheherekea, sio kama hii ni mara ya kwanza kwa Liverpool kuwa juu ya ligi. Sidhani kama wamiliki watasherehekea. Mimi hakika sitasherehekea, na wachezaji pia hawatafanya hivyo.”
Liverpool inaingia kwenye wiki ya mechi ngumu na baada ya kucheza na Southampton wikiendi hii itakutana na Real Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa kabla ya kuikaribisha Man City katika dimba la Anfield.
“Siwezi kuzungumzia ubingwa kwa sasa, nitakuwa najichosha. Nitajikita katika kuzungumzia mchezo ujao ambao ndio ninatakiwa niukabili kwa sasa. Nimesema mara nyingi kuwa katika Ligi Kuu England, utofauti wa ubora baina ya timu ni mdogo sana, hivyo lolote linaweza kutokea. Msimu uliopita nilikuwa nafuatilia ligi na kulikuwa na wakati Man City ilikuwa nyuma ya Arsenal kwa pointi nane (ilikuwa msimu wa 2022-23), hivyo hakuna haja ya kusherehekea kabisa kwa sasa. Timu hizi kama Man City, Arsenal na Chelsea na hata Manchester United na nyingine zote zina uwezo wa kupata matokeo ya mfululiz kama tulivyofanya sisi.”