Slot apongezwa kumpiga benchi Mo Salah!
Muktasari:
- Tangu mwanzoni mwa msimu huu, Mo Salah amekuwa akikosolewa kutokana na kiwango chake kuporomoka na hivyo kukifanya kikosi cha Liverpool kuvuna matokeo mabovu uwanjani.
LIVERPOOL ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot amepongezwa kwa uamuzi wake wa kumpiga benchi supastaa Mohamed Salah akielezwa kufanya hivyo kutamsaidia winga huyo kurejea kwenye makali yake.
Tangu mwanzoni mwa msimu huu, Mo Salah amekuwa akikosolewa kutokana na kiwango chake kuporomoka na hivyo kukifanya kikosi cha Liverpool kuvuna matokeo mabovu uwanjani.
Mo Salah hayupo vizuri msimu huu, lakini hilo si kwake pekee bali kuna wachezaji kibao katika kikosi cha Liverpool, wamekuwa wakicheza chini ya kiwango. Sasa vidole vyote vinaelekezwa kwa Mo Salah, ambaye anaonekana kama tatizo kwenye kuifanya Liverpool kucheza kwa ubora mkubwa, kwa sababu uwepo wake uwanjani kunawanyima nafasi wachezaji wengine ambao pengine wangefanya kitu cha maana kwa wababe hao wa Anfield.
Kulikuwa na viwango vya hovyo pia kwa mastaa Florian Wirtz na Alexander Isak, lakini dhidi ya West Ham United, wawili hao walionyesha kiwango bora kwa mara ya kwanza tangu walipotua Liverpool. Walikuwa kwenye viwango bora katika mechi hiyo ya West Ham.
Mo Salah amekosa msaada kwenye mechi zilizopita, licha ya kwamba alikuwa mchezaji pekee wa Liverpool, aliyekuwa tishio kwenye mechi ya kichapo cha mabao 3-0 kwenye Ligi Kuu England dhidi ya Nottingham Forest. Lakini, alicheza kwa kiwango cha hovyo sana katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSV Eindhoven, ambapo alishindwa kurudi nyuma kukaba kuzuia bao la pili lililofungwa na Wadachi hao kwenye ushindi wa 4-1 na hivyo, kocha Slot amechukua hatua.
Baada ya Liverpool kuonyesha kiwango bora kwenye mechi dhidi ya West Ham, kikosi hicho cha kocha Slot kilikuwa na uwiano mzuri uwanjani na sasa Mo Salah anaweza kujikuta kwenye wakati mgumu wa kurejea kwenye kikosi kinachoanza, hasa kwa kuanzia mechi dhidi ya Sunderland itakayopigwa Anfield. Lakini, inaaminika kwamba Slot uamuzi wa kumweka Salah benchi, utamsaidia mchezaji huyo kupumzika na kurudi uwanjani kwa nguvu mpya.
Mo Salah, 33 anahitaji kupumzika. Si kupumzika kwa ajili ya msimu huu, bali mapumziko ya kumfanya arudi kwenye viwango bora kutokana na kutumika sana.
Staa huyo si kwamba anahitaji kupumzika baada ya kuchezea klabu yake mechi 18 msimu huu, bali anahitaji kupumzika baada ya kuichezea timu hiyo mechi 419 katika misimu minane.
Staa huyo amecheza mechi 109 kwenye kikosi cha Misri. Hiyo ina maana, staa huyo ambaye atatimiza umri wa miaka 34, Juni mwakani, amecheza karibu mechi 800 kwenye klabu na timu ya taifa. Kwa kipindi hicho hicho alichochezea klabu na timu ya taifa, majeruhi na ugonjwa vilimfanya Mo Salah ashindwe kujumuishwa kwenye timu katika mechi 38 tu, huku tatu zilikuwa kwenye kipindi cha janga la Uviko 19. Hiyo ni rekodi ya kipekee kabisa na mzigo wa mechi nyingi alizocheza Mo Salah, ambaye sasa anahitaji kupumzika ili kuwa na kuchaji betri.
Atakaporejea kutoka kwenye majukumu ya timu ya taifa huko kwenye mashindano ya Afcon 2025, kitakuwa kitu kinachosubiriwa kwa hamu kuona Salah atarudi kwa mtindo upya katika mchakamchaka wa kuisaidia Liverpool katika mzunguko wa pili wa ligi msimu huu. Liverpool bado haijatoka kwenye ramani mazima katika harakati zao za kutetea ubingwa wa EPL.
Na sasa kitu anachojutia kocha Slot ni kushindwa kuwapa nafasi ya kucheza wachezaji wake wote kwenye kikosi kwa msimu uliopita na badala yake aling’ang’ania wachezaji walewale na kuwafanya wachoke kwa kucheza mechi nyingi.