Didi Hamann: Slot siku zake zinahesabika
Muktasari:
- Liverpool imepoteza mechi tisa kati ya 12 za hivi karibuni na iliruhusu mabao matatu katika kila mechi kwenye mechi tatu za mwisho.
LIVERPOOL, ENGLAND: MCHEZAJI wa zamani wa Liverpool, Didi Hamann amesema kocha wa timu hiyo Arne Slot amepoteza ushawishi kwa wachezaji na mwisho wake unanukia katika viunga hivyo vya Anfield.
Liverpool imepoteza mechi tisa kati ya 12 za hivi karibuni na iliruhusu mabao matatu katika kila mechi kwenye mechi tatu za mwisho.
Kupoteza kwa mabao 4-1 nyumbani dhidi ya PSV Eindhoven Jumatano kulizidisha hofu kuhusu mustakabali wa Slot juu ya ajira yake katika kikosi cha majogoo hao.
Hamann, aliyewahi kushinda Ligi ya Mabingwa na Liverpool mwaka 2005, anaamini muda wa Slot unakaribia kuisha.
Akizungumza na Sky Germany amesema: "Ninaamini Arne Slot amepoteza ushawishi kwa wachezaji, timu imegawanyika, kila mtu anafanya anachotaka. Liverpool itakuwa na wakati mgumu sana msimu huu hata kumaliza ndani ya nafasi nne za juu katika EPL. Sioni kama itarudi katika hali yake hivi karibuni. Hali ni ngumu sana kiasi kwamba hadi kufikia sasa mabosi wanajadili uwezekano wa kumwondoa kocha. Mwisho wa Slot uko karibu. Sikuwahi kuwaza angekuwa na wakati huu muda kama huu kwa kile ambacho alikifanya msimu uliopita."
Mabosi wa Liverpool walionekana kuwa na imani sana na Slot, kiasi cha kumpa kiasi kikubwa cha pesa katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi kwa ajili ya kufanya usajili wa Alexander Isak na Florian Wirtz waliogharimu takriban Pauni 240 milioni, lakini bado hawajaonekana kuonyesha kiwango kilichotarajiwa.