Kwanza Klopp, kisha Enrique
Muktasari:
- Kwa sasa lisemwalo ni kwamba Mjerumani Klopp ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kurudi Anfield kufanya kazi kipindi cha mpito ili kujiandaa na msako wa kocha mpya.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL itamgeukia kocha wake wa zamani, Jurgen Klopp kupiga mzigo upya huko Anfield itakapoamua kumfuta kazi Arne Slot kabla ya kutafuta namna kumpata kocha inayemtaka ambaye ni Luis Enrique.
Kwa sasa lisemwalo ni kwamba Mjerumani Klopp ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kurudi Anfield kufanya kazi kipindi cha mpito ili kujiandaa na msako wa kocha mpya.
Klopp aliachana na Liverpool majira ya kiangazi 2024 na Slot akachukua mikoba. Mdachi huyo, Klopp alitamba ndani ya muda mfupi tu baada ya kutua Anfield, ambapo aliongoza kushinda Ligi Kuu England msimu wa kwanza, lakini kwa sasa mambo yametibuka, timu imekumbana na vichapo tisa katika mechi 12 za michuano yote.
Hata hivyo, Slot hayupo kwenye presha ya kupoteza kibarua. Lakini, kama hilo litatokea, basi mabosi wa Anfield bila shaka watarudi kwa Klopp kumpa mikoba hadi mwishoni mwa msimu.
Kinachoelezwa ni kwamba Liverpool ipo kwenye mchakato wa kumfukuzia kocha wa PSG, Luis Enrique, wakimtaka akapige mzigo huko Anfield.
Kinachoripotiwa ni kwamba kuna majadiliano yanaendelea kwa sasa miongoni mwa mabosi wakubwa wa Liverpool juu ya hatima ya kocha Slot. Mabosi hao wamedai kwamba wana wasiwasi kocha Slot amepoteza nguvu kwenye vyumba vya kubadilishia vya timu hiyo.
Baada ya Liverpool kuchapwa 4-1 na PSV Eindhoven kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Slot alisema: “Kama unapoteza mara nyingi, watu wataanza kulizungumzia hilo. Ninapata sapoti kubwa sana kutoka huko juu. Niko sawa kwenye nafasi yangu.”
Liverpool itarejea mzigoni Jumapili katika kipute matata kabisa cha Ligi Kuu England dhidi ya West Ham United kwenye Uwanja wa London. Kipigo kwenye mechi hiyo kutazidisha presha kwenye usalama wa kibarua cha kocha Slot.
Kufuatia matumizi ya Pauni 420 milioni kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi inamfanya Slot kuwa kwenye wakati mgumu wa kutoa maelezo kwanini mambo hayaendi. Kiasi hicho cha pesa kilichotumika, Pauni 125 milioni ilitolewa kumsajili Alexander Isak kutoka Newcastle.