Majeruhi Liverpool, Slot kichwa kinauma
Muktasari:
- Leoni, mwenye umri wa miaka 18, alivunjika goti Jumanne wakati Liverpool iliposhinda 2-1 dhidi ya Southampton kwenye Uwanja wa Anfield.
LIVERPOOL, ENGLAND: BAADA ya beki chipukizi Giovanni Leoni kupatwa na majeraha katika mechi ya mashindano ya Carabao dhidi ya Southampton, kocha wa Liverpool, Arne Slot sasa kichwa kinauma.
Leoni, mwenye umri wa miaka 18, alivunjika goti Jumanne wakati Liverpool iliposhinda 2-1 dhidi ya Southampton kwenye Uwanja wa Anfield.
Beki huyo wa kati sasa anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa miezi kadhaa baada ya ripoti ya daktari kutoka na kuanza matibabu.
Nyota huyo wa kimataifa wa Italia anayeichezea timu ya vijana ya taifa hilo anakabiliwa na safari ndefu na ngumu ya kurejea dimbani kabla ya msimu kumalizika.
Leoni alionyesha kiwango bora katika dakika zote alizocheza dhidi ya Southampton kabla ya kuanguka vibaya na kuumia.
Madaktari walimpa huduma ya kwanza kiwanjani kabla ya kumbeba na kumpeleka nje kwa machela, huku akiwa analia na nafasi yake ikachukuliwa na Milos Kerkez.
Jeraha alilopata mchezaji huyo wa zamani wa Parma linamweka katika wakati mgumu kocha Arne Slot kwa sababu ya uhaba uliopo kwa wachezaji katika safu ya ulinzi.
Ibrahima Konate na Joe Gomez wamekuwa wakisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara kwa miaka ya hivi karibuni jambo ambalo linasababisha hatari endapo mmoja wao ataumia au wote kwani mabeki wa kati pekee waliobakia watakuwa ni Virgil van Dijk na Rhys Williams.
Ikiwa Konate na Gomez watakumbwa na majeraha, kocha huyo Mholanzi atalazimika kuwahamisha nafasi viungo wake Wataru Endo na Ryan Gravenberch kwenda kucheza kama mabeki wa kati.
Ukosefu huo wa wachezaji katika safu ya ulinzi ndio sababu kubwa iliyowafanya Liverpool kupambana kwa nguvu zote kumsajili Marc Guehi wa Crystal Palace siku ya mwisho ya dirisha la usajili.
Hata hivyo, uhamisho wa Guehi kwenda Anfield uligonga mwamba kwa sababu Palace hawakuwa na mchezaji mbadala wa kuziba pengo lake.