Slot ahuzunika kisa Luis Diaz, ilaa....
Muktasari:
- Nyota huyo wa kimataifa wa Colombia alikamilisha uhamisho wa Pauni 65.5 milioni kwenda kwa mabingwa hao wa Bundesliga akisaini mkataba wa hadi 2029.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot anaamini Liverpool imefanya “biashara nzuri” kwa kupata faida kupitia mauzo ya Luis Diaz kwenda Bayern Munich lakini amesikitishwa na kuondoka kwake kutokana na mchango katika kikosi.
Nyota huyo wa kimataifa wa Colombia alikamilisha uhamisho wa Pauni 65.5 milioni kwenda kwa mabingwa hao wa Bundesliga akisaini mkataba wa hadi 2029.
Diaz, mwenye umri wa miaka 28, alitangazwa kuwa hauzwi na Liverpool mwanzoni mwa dirisha la usajili, lakini hatimaye klabu ikashawishika kumuuza baada ya mchezaji mwenyewe kuomba kuondoka na ofa ambayo Bayern iliiweka mezani.
Winga huyo alichangia sana katika ushindi wa taji la Ligi Kuu msimu uliopita chini ya Slot, lakini amekuwa akihusishwa kuondoka tangu mwaka jana licha ya kuwa bado alikuwa na mkataba.
Uhamisho huo unamaliza kipindi chake cha miaka mitatu na nusu cha kuwa Anfield, tangu alipojiunga akitokea Porto mwaka 2022 kwa dau la Pauni 37 milioni.
Slot amekiri kuwa na huzuni kumwona Diaz anaondoka, hasa baada ya mchezaji huyo kufunga mabao 13 na kutoa pasi za mabao saba msimu uliopita wa Ligi Kuu England.
Hata hivyo, kocha huyo wa kimataifa wa Uholanzi ana imani na uwezo wa timu kuleta wachezaji wapya kupitia pesa za mauzo zilizopatikana kutoka kwa Diaz.
“Luis ni mchezaji tuliyechukua naye ubingwa ni mchezaji mzuri sana,” alisema Slot. “Daima ni jambo la kusikitisha kumuona mchezaji kama huyo akiondoka, lakini kwa upande mwingine, tumemuuzia kwa pesa nyingi, na kama unavyojua klabu hii imekuwa ikileta wachezaji wazuri kwa miaka mingi. Sehemu ya mkakati wetu pia ni kwamba wakati fulani tunalazimika kuuza mchezaji kwa ajili ya mapato. Nadhani tumefanya biashara nzuri kwa kumbakiza Diaz kwa miaka kadhaa, kisha tukamuuzia kwa faida kubwa. Diaz alikuwa mchezaji mzuri kuwahi kufanya naye kazi kila siku alikuwa na tabasamu usoni. Nitamkumbuka kama mtu wa kupenda kufurahi na mshindi wa taji la EPL.”
Slot anaamini tayari ana machaguo kadhaa kwa ajili ya kujaza pengo lililoachwa na Diaz na ametaja jina la chipukizi Rio Ngumoha, ambaye ameonyesha kiwango kizuri katika maandalizi ya msimu, pamoja na Cody Gakpo na Florian Wirtz.