Haaland apokelewa, mzigo wazuo gumzo
Muktasari:
- Norway ilimaliza safari yake kwa kufungwa mabao 2-1 na England baada ya dakika za nyongeza, huku Jude Bellingham akifunga mabao yote mawili yaliyowavusha Waingereza kwenda nusu fainali.
OSLO, NORWAY: NYOTA wa Manchester City, Erling Haaland, amerejea nchini Norway akipokelewa kama shujaa baada ya kuiongoza timu yake kufika robo fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998.
Norway ilimaliza safari yake kwa kufungwa mabao 2-1 na England baada ya dakika za nyongeza, huku Jude Bellingham akifunga mabao yote mawili yaliyowavusha Waingereza kwenda nusu fainali.
Licha ya maumivu ya kuondolewa, Haaland alikuwa mmoja wa mastaa wa mashindano hayo baada ya kufunga mabao saba katika mechi tano.
Mapokezi ya timu hiyo jijini Oslo yalikuwa ya aina yake, ndege yao ikipokelewa kwa maji yaliyomwagwa na magari ya zimamoto huku maelfu ya mashabiki wakijitokeza kuwashangilia.
Kilichovuta zaidi macho ni Haaland kushuka akiwa amebeba kinyago cha mnyama aina ya ‘raccoon’ kilichoshika chupa tupu ya whisky.
Inadaiwa alikinunua katika duka moja jijini Dallas kwa pauni 560, na bidhaa hiyo sasa imeisha sokoni kutokana na umaarufu wake.
Baadaye kikosi hicho kilipokelewa na Mfalme Harald pamoja na Malkia Sonja kabla ya kufanya gwaride la ushindi kupitia mitaa ya Oslo.
Wakati huohuo, FIFA imefuta rasmi malalamiko ya Norway kuhusu bao la kwanza la Bellingham. Uchunguzi wa kamera maalumu na mfumo wa teknolojia ya mpira umeonyesha kuwa mpira haukugusa nyaya za kamera kama walivyodai Wanorway, hivyo bao hilo lilikuwa halali.